July 12, 2022

WADAU WATAKA BODI HURU YA ITHIBATI YA HARARI

 

NA MWANDISHI WETU


MJUMBE wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Nevile Meena  amesema Bodi ya Ithibati ya Habari ikiwa itaundwa na Serikali  basi itakosa uhuru wa kufanya uamuzi pale malalamiko yatakapoihusu yenyewe (serikali).
 

Meena ambaye ni Katibu Mstaafu wa TEF amesema, ili kukwepa hilo na kutenda haki kwa vyombo vyote vya habari nchini, hakuna budi kwa Bodi ya Ithibati ya Habari kuundwa na kusimamiwa na wanataaluma haswa wanahabari.

 

Kauli hiyo imetolewa jijini Dar es Salaam  leo wakati wakizungumza  juu ya Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016.

 

“Bodi ya Ithibati ya Habari  inapaswa kuundwa na wanataaluma wenyewe kwa kuwa ikiwa itasimamiwa na serikali, itakosa uhuru wa kuamua.

 

“Serikali ikiwa na malalamiko nayo inakwenda kulalamika kwenye bodi na wala haipaswi kutoa maelekezo,” amesema Meena.

 

Kwa upande wake Mhariri wa Gazeti la Raia Mwema Joseph Kulangwa  amebainisha kuwa ikiwa serikali itataka wanaowaandika vizuri tu, ndio wahalalishwe kufanya kazi hiyo basi hapo hakutakuwa na uhuru.

 

Aidha Kulangwa ameeleza  kuwa, tasnia mbalimbali nchini zimeunda na kusimamia bodi zao wenyewe bila maelekezo ama kuingiliwa na serikali, na kushangazwa na serikali kupendekeza kuunda bodi hiyo badala ya kuwaacha wanataaluma wa habari kuunda na kusimamia bodi hiyo.

 

“Tasnia inatakiwa kujidhibiti yenyewe kama wanavyofanya wanasheria na wengine. Serikali ikiwa ndiye mdhibiti wa bodi hiyo, kutakuwa na upendeleo kwa magazeti yanayoitwa ya umma” amebainisha Kulangwa.

 

Naye Mhariri wa Jarida la Tz & Beyond na PANAROMA Jimmy Charles ameongeza  kuwa, iwapo serikali itaunda bodi hiyo, itajihakikishia uhuru wa Habari kutuama mikononi mwake.

 

“Serikali ikiundwa bodi kama inavyoelekezwa na sheria, basi uhuru wa habari utaendelea kutuama kwenye mikononi yake (serikali).

 

“Ikumbukwe kuwa, kwa sasa serikali ndio mwamuzi wa mwisho kwa maana ya kuwa ndio mlalamikaji, msikilizaji na hakimu kwa wakati mmoja.

 

“Tasnia ya Habari inahitaji bodi huru isiyosimamiwa na Serikali.”ameeleza Charles.

 

Mei 31,2021, aliyekuwa Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Innocent Bashungwa alieleza kuwa Serikali inaendelea na taratibu za kuanzisha Bodi ya Ithibati itayokuwa na jukumu la kutoa ithibati na vitambulisho kwa wanahabari wenye sifa.

 

Bashungwa alitoa kauli hiyo wakati akiwasilisha makadiro ya Mapato na Matumizi ya wizara hiyo kwa mwaka wa fedha 2021/2022.

 

Aidha alisema, Sheria ya Huduma za Habari ya mwaka 2016, inaelekeza kuanzishwa kwa Bodi ya Ithibati, Baraza Huru la Habari pamoja na mfuko wa mafunzo kwa wanahabari.

 

“Kwa sasa wizara inaendelea na taratibu za kuanzisha bodi hii, na kuongeza Baraza Huru la Habari litaundwa baada ya Bodi ya Ithibati kuanza kazi.”alieleza Bashungwa.

 

Kwa upande wa Jaji Eliezer Feleshi ambaye ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), alisema ni vizuri kwa Bodi ya Ithibati ya Habari ikaundwa na kusimamiwa na wanahabari wenyewe.

 

Jaji Feleshi alitoa maoni hayo Mei 13,2022 wakati alipokutana na wadau wa habari ofisini kwake bungeni, jijini Dodoma. wakiongozwa na Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF) Deodatus Balile.

No comments:

Post a Comment

Pages