August 14, 2022

DKT. MPANGO APONGEZA CRDB BANK MARATHON 2022 KUKUSANYA BILIONI 1.05 KUSAIDIA JAMII

‘Wakimbiaji waondoka na zawadi zaidi ya shilingi milioni 100’

Wakimbiaji wa CRDB Marathon 2022 wakishiriki mbio za Km 5 zilizoanzia na kuishia katika viwanja vya Farasi Oysterbay jijini Dar es Salaam leo 14, 2022.
Wakimbiaji wa CRDB Marathon 2022 wakishiriki mbio za Km 5 zilizoanzia na kuishia katika viwanja vya Farasi Oysterbay jijini Dar es Salaam leo 14, 2022.
 
Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, akimkabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni 200 Afisa Mtendaji Mkuu wa Hospitali ya CCBRT, Brenda Msangi,
 Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango, akimkabidhi mfano wa hundi ya shilingi milioni 250 mwakilishi wa Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Prof. Mohammed Janabi (katikati). Kushoto ni Rais mstaafu Dk. Jakaya Kikwete, wa pili kushoto ni Mkurugenzi Mtendaji Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela na kulia ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Bima ya Sanlam. 

Dar es Salaam 14 Agosti 2021 – Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Mpango ametoa pongezi kwa mbio za hisani za kimataifa zinazoandaliwa na Benki ya CRDB “CRDB Bank Marathon” kwa kufikisha lengo la kukusanya shilingi bilioni 1 kwa ajili ya kusaidia jamii.

 

Dkt. Mpango ametoa pongezi hizo wakati akikabidhi mfano wa hundi kwa Taasisi ya Moyo ya Jakaya na Hospitali ya CCBRT muda mchache baada ya kukamilika kwa mbio hizo ambazo zilishirikisha zaidi ya wakimbiaji 6,200.

 

Alipongeza uamuzi wa Benki ya CRDB kuendelea kusaidia upasuaji wa watoto wenye magonjwa ya moyo, pamoja na wazo jipya la kusaidia upatikanaji wa huduma salama za uzazi kwa wakinamama wenye ujauzito hatarishi alibainisha.

 

“Afya ya mama na mtoto ni moja ya maeneo yanayopewa kipaumbele kikubwa katika Sera ya Afya. Ninafarijika kuona mbio hizi zinasaidia kuimarisha eneo hili kwa kufanikisha upatikanaji wa huduma ya matibabu kwa watoto na wakinamama,” aliongezea.

 

Dkt. Mpango alisema fedha hizo zilizokusanywa zitasaidia kupunguza makali ya gharama kwa ajili ya upasuaji wa moyo na huduma za uzazi kwa wakinamama  wenye ujauzito hatarishi ambazo watu wengi hawawezi kuzimudu pamoja na Serikali kutoa ruzuku ya asilimia 80.

 

Dkt.  Mpango alisema Serikali inaunga mkono na kufurahishwa sana na ubunifu wa taasisi za kizalendo kama Benki ya CRDB kusaidia sekta za kijamii kama vile afya, elimu, mazingira, na uwezeshaji kwa vijana na wanawake.

 

Viongozi mbalimbali waliongozana na Makamu wa Rais kushiriki mbio hizo ikiwamo Rais Mstaafu wa Awamu ya Nne, Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete, Naibu Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano, Mheshimiwa Mussa Azan Zungu, Naibu Waziri wa Utamaduni, Sanaa, na Michezo, Mheshimiwa Pauline Gekule, na Waziri wa Michezo Zanzibar, Mheshimiwa Tabia Mwita Maulid.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela alibainisha kuwa mbizo za mwaka huu zimevuka lengo la ukusanyaji wa Shilingi bilioni 1, akitoa shukrani kwa makampuni, na taasisi zilizojitokeza kushirikiana na benki hiyo, pamoja na wakimbiaji waliojitokeza kutoka ndani na nje ya nchi.

 

“Kati ya fedha zote Sh bilioni 1.05 zilizopatikana katika msimu huu wa tatu wa CRDB Bank Marathon, Shilingi Milioni 250 zimeelekezwa JKCI, Sh milioni 220 zimeenda Hospitali ya CCBRT, huku fedha iliyobaki kuelekezwa kusaidia kampeni ya mazingira ya Pendezesha Tanzania, na resi za ngalawa kule Zanzibar kukuza utamaduni,” alisema Nsekela.

 

Nsekela aliwashukuru Mkurugenzi Mtendaji wa JKCI, Prof. Mohammed Janabi na Mkurugenzi Mkuu wa Hospitali ya CCBRT, Brenda Msangi kwa ushirikiano wao huku akiweka mkazo kuwa kauli mbiu ya benki hiyo isemayo “Kasi Isambazayo Tabasamu” imefanikiwa kutokana na mchango wao wa dhati.

 

Katika mbio hizo washiriki takribani 60 waliofanya vizuri wameweza kujishindia zawadi zenye jumla ya thamani ya shilingi milioni 100. Zawadi hizo zinaifanya CRDB Bank Marathon kuwa mbio zinazolipa zaidi nchini ambapo washindi wa 42km kwa wanawake na wanaume wameondoka na kitita cha Sh milioni 10 kila mmoja.

 

Akitangaza matokeo ya mbio hizo, Mkurugenzi wa Mawasiliano Benki ya CRDB, Tully Mwambapa alisema kwa upande wa kilometa 42, Joseph Munywoki raia wa Kenya ameibuka kinara akitumi muda wa 02:14:56, wakati Shoron Kosgei raia wa Kenya aliibuka mshindi kwa upande wa wanawake akitumia muda 02:33:56.

 

Kwa mbio za kilometa 21, mshindi kwa upande wa wanaume alikuwa Samwel Mailu raia wa Tanzania akitumia muda wa 01:02:04, kwa upande wa wanawake mshindi alikuwa Agnes Ngolo raia wa Tanzania baada ya kutumia muda wa 01:09:16.

 

Katika 10km, mshindi kwa upande wa wanaume alikuwa Gabriel Geay raia wa Zambia alitumia muda wa 00:28:16, kwa wanawake Maysellina Issa raia wa Tanzania ameshika nafasi ya kwanza baada ya kutumia muda wa 00:33:52.

 

Katika mashindano ya mbio za baiskeli kilometa 65, Richard Laizer raia wa Tanzania aliibuka mshindi kwa upande wa wanaume kwa kutumia muda wa 01:39:24, upande wa wanawake Julia Miringu raia wa Tanzania ameibuka mshindi baada ya kutumia muda wa 01:45:11.

 

Kati ya washiriki 6,200 walioshiriki katika CRDB Bank Marathon mwaka huu asilimia 79 ya ni Watanzania, wakimbiaji wa kimataifa walioshiriki ni zaidi ya 1,300.

No comments:

Post a Comment

Pages