August 01, 2022

NMB yatoa Milioni 60 Maonyesho ya Nanenane Mbeya.


MKUU wa Wilaya ya Mbeya Dk. Rashid Mohamed Chuachua , akipokea hundi ya Shilingi Milioni 60 kutoka Meneja wa Benki ya NMB Kanda Nyanda za Juu Straton Chilongola akimwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, ikiwa ni sapoti ya kuwezesha maonesho ya Nane Nane yanayofanyika Kitaifa Mkoani Mbeya mwaka huu 2022. Benki ya NMB ni mmoja ya wadhamini wakuu wa maonyesho hayo ya NaneNane.



Na Mwandishi Wetu, Mbeya


Benki ya NMB imeendelea kuunga mkono serikali katika kufanikisha ufanyikaji wa maonyesho ya sikukuu ya wakulima kitaifa (Nanenane) ambapo jana imekabishi kiasi cha Sh. Milioni 60 kwa ajili ya maonyesho hayo.

Udhamini huo unaifanya benki hiyo kufikisha kiasi cha Sh. Milioni 195 ambazo imetoa kwa kipindi cha Miaka mitano katika kufanikisha shughuli za manyesho hayo kitaifa.

Katika hafla ya kukabidhi hundi ya fedha hizo iliyofanyika mjini Mbeya Meneja wa NMB kanda ya nyanda za juu Kusini Straton Chilongola amesema kuwa benki hiyo imetoa kiasi cha fedha kwa ajili ya kufanikisha shughuli mbalimbali za maonyesho hayo.

“ Kwetu kusaidia sekta ya kilimo ni fahari yetu kwani kupitia kilimo, benki hii imekuwa ikifanya biashara kubwa ambayo pia imechangia sana ukuaji wa sekta ya kilimo nchini na Mbeya kwa ujumla,” amesema Chilongola.

Amesema kuwa kwa miaka mitano ambayo maonyesho ya Nane Nane yamefanyika nchini, NMB imetoa udhamini wa zaidi ya shilingi milioni 195 fedha ambazo benki hiyo inaamini zinachangia pakubwa katika kufanikisha maonyesho hayo muhimu kwa taifa.

Aidha Chilongola amesema kuwa katika kuunga mkono juhudi za Rais wa Awamu ya sita, Samia Suluhu Hassan, Mchango wa NMB kama benki wakujenga Uchumi imara kupitia kilimo na ufugaji ni kuwa Ndani ya miaka minne, wamefungua zaidi ya akaunti 644,034 za wakulima nchi nzima.

Mkuu wa Wilaya ya Mbeya ambaye alipokea hundi ya fedha hizo kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa huo Juma Homera aliishukuru Benki ya NMB kwa kutoa kiasi hicho cha fedha ambacho alieleza kitawezesha maonyesho kufanyika kwa ubora.

“Kwa niaba ya Mkuu wa Mkoa, nawashukuru sana viongozi wa Benki ya NMB kwa udhamini wao, tunaamini utatusaidia kuboresha maonyesho yetu,” alisema Dk.Chuachua. 


Alisema tayari maonesho hayo yameanza na hivyo kuwataka wananchi wakiwemo wajasiriamali kutembelea mabanda na kwamba zipo kamati zinazoratibu taratibu mbalimbali kwenye maonyesho hayo.


No comments:

Post a Comment

Pages