Dotto Mwaibale na Thobias Mwanakatwe, Singida
ZOEZI la Sensa ya Watu na Makazi limeendelea vizuri katika Mkoa wa Singida
ambapo makarani walianza kazi ya kuhesabu watu katika maeneo maalum kama nyumba
za kulala wageni na vituo vya mabasi na kupata ushirikiano wa kutosha.
Mkuu wa Mkoa wa Singida, Peter Serukamba, akizungumza na waandishi wa
habari baada ya kushiriki sensa, alisema kutokana na uhamasishaji wa kutosha
uliofanyika wananchi wamekuwa wakitoa ushirikiano mzuri kwa makarani wa sensa.
"Maeneo ambayo yalikuwa na changamoto kidogo kama Wilaya ya Singida
vijijini,mpaka wa Mkoa wa Manyara na mpaka wa Mkoa wa Dodoma tumeongea na
wananchi na wamekubali kuhesabiwa," alisema.
Serukamba amewaomba wananchi wanapotoka waache namba za simu na taarifa
sahihi majumbani mwao ili makarani watakapofika wawatafute na kushirikia zoezi
la kuhesabiwa.
Naye Mwenyekiti wa Chama Cha
Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Singida, Alhaji Juma Killimbah, alisema wananchi
watakapojitokeza kuhesabiwa watakuwa wameisaidia serikali inayoongozwa na CCM
kupanga mipango yake ya maendeleo.
"Sisi CCM huwa tunatengeneza ilani ya chama kulingana na idadi ya watu
kwa hiyo tunawaomba wananchi wajitokeze kuhesabiwa na kwa jinsi serikali ya
Mkoa wa Singida ilivyofanya uhamasisha mkoa utafanikiwa katika zoezi
hili," alisema.
Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Singida, Mhandisi Paskas Mulagiri,
alisema kulikuwa na changamoto iliyojitokeza katika baadhi ya kata ambapo
wananchi walisema hawatahesabiwa kwasababu tu mipaka ya sensa haiendani na
mipaka ya kiutawala.
Alisema kutokana na changamoto hiyo, Kamati ya Ulinzi na Usalama
ilishughulikia tatizo hilo kwa kutembelea kata husika kuzungumza na wananchi
ambao wameelimishwa na wamekubali kuhesabiwa.
"Natoa wito kwa wananchi watambue kuwa mipaka ya sensa si mipaka ya
kiutawala mipaka hii imetengwa kwa ajili ya maeneo ya sensa ambayo watu wa
takwimu wanaitumia kujua idadi ya watu," alisema.
Maeneo mengi ya mji wa Singida wananchi wameonekana wakiwa majumbani mwao kusubiri makarani kuhesabiwa na hata maeneo ya biashara ushirikiano kwa makarani umekuwa mzuri.
No comments:
Post a Comment