August 29, 2022

SERIKALI KUSHIRIKISHA WADAU BEI ELEKEZI ZA MIFUGO

Na Mbaraka Kambona, Geita


Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Mhe. Mashimba Ndaki amesema Serikali ipo kwenye mchakato wa kushirikisha wadau wa sekta ya mifugo kupanga bei elekezi za kuuzia mifugo katika minada ili kuwawezesha wafugaji na  wafanyabiashara kuuza mifugo yao kwa bei ambayo wao watakuwa wameshiriki kuipanga.

Alitoa kauli hiyo wakati alipotembelea na kukagua maendeleo ya ujenzi wa mnada wa Kimataifa  wa Buzirayombo unaojengwa Wilayani Chato, Mkoani Geita Mwishoni mwa wiki.

Alisema suala la kuwa na bei elekezi, Serikali inalifanyia kazi na tayari Wataalam walishaandaa na hatua iliyopo sasa ni ya kuwashirikisha wafugaji na wafanyabiashara wa mifugo ili kwa pamoja waweze kukubaliana na kuja na bei ambayo itakuwa imeridhiwa na pande zote.

"Bei elekezi ikitoka ndio itakuwa mahali pa kuanzia na kwenda juu, hivyo tunalifanyia kazi suala hilo na muda sio mrefu tutato muelekeo wa jambo hilo", alisema

Aliongeza kwa kusema kuwa sambamba na bei elekezi Serikali inataka sasa mifugo yote nchini ianze kupimwa kwa kilo kama ambavyo mifugo itapimwa kwa kilo katika mnada huo wa kisasa wa Buzirayombo.

"Minada yetu yote tutakayoizindua safari hii tunataka iwe na mizani ya kupimia uzito wa mifugo na hili tunataka lifanyike pia katika minada yote ya awali inayomilikiwa na Halmashauri zetu hapa nchi ili tuondokane na vitendo vya kuwapunja wafugaji wetu", aliongeza 

Kwa upande wake, Mbunge wa Jimbo la Chato, Mhe. Medard Kalemani aliishukuru Serikali kupitia Wizara ya Mifugo na Uvuvi kwa kujenga mnada huo wa kimataifa Wilayani humo huku akiongeza kwa kuiomba  kuhakikisha mradi huo unamalizika haraka ili wananchi wa Kanda ya Ziwa na maeneo mengine waanze kuona matunda yake.

No comments:

Post a Comment

Pages