Waziri wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba (Mb) (katikati), akiongoza ujumbe wa Tanzania kwenye mkutano wa 6 wa Kamati ya Pamoja ya Uchumi, Ufundi na Biashara kati ya Tanzania na Jamhuri ya Watu wa China, uliofanyika kwa njia ya mtandao Jijini Dar es Salaam, wakimsikiliza Naibu Waziri wa Biashara wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe. Qian Keming. Kulia ni Kamishna Msaidizi wa Idara ya Fedha za Nje Bw. Robert Mtengule na kushoto ni Kamishna Msaidizi pia wa Idara ya Fedha za Nje, Bw. Melkizedeck Mbise, wote kutoka Wizara ya Fedha na Mipango.
Na Benny Mwaipaja, WFM, Dar es Salaam
WAZIRI
wa Fedha na Mipango, Mhe. Dkt. Mwigulu Lameck Nchemba, amesema kuwa
Serikali ya Tanzania inatarajia kunufaika na mpango wa msaada wa miaka
mitatu utakaogharimu dola za Marekani bilioni 30, ulioahidiwa na Rais wa
jamhuri ya Watu wa China Mheshimiwa XI JINPIN, wa kuzisaidia nchi za
Afrika kukabiliana na umasikini.
Dkt.
Nchemba ametoa kauli hiyo Jijini Dar es Salaam alipofanya mazungumzo
kwa njia ya mtandao na Naibu Waziri wa Biashara wa Jamhuri ya Watu wa
China Mhe. Qian Keming, wakati wa mkutano wa 6 wa Kamati ya Pamoja ya
Uchumi, Ufundi na Biashara kati ya Tanzania na China.
Alisema
kuwa msaada huo ulioahidiwa na Rais wa Nchi hiyo Mheshimiwa XI Jinping,
Mwezi Novemba mwaka 2021, Mjini Dakar, Senegal, kupitia mpango wa
ushirikiano wa China na Afrika wa mwaka 2035, utasaidia upatikanaji wa
fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo hapa
nchini.
Dkt.
Nchemba alisema kuwa kupitia mpango huo, miradi 9 imekusudiwa
kutekelezwa katika sekta za afya, kilimo, kutokomeza umasikini,
kuendeleza biashara, uwekezaji, ubunifu wa teknolojia, kukabiliana na
mabadiliko ya Tabianchi, kujenga uwezo na uhusiano wa moj kwa moja wa
watu wa nchi hizo mbili.
“Tumewasilisha
China miradi kadhaa ya kimkakati na kipaumbele ili nchi hiyo iweze
kuisadia Tanzania kupata misaada na mikopo nafuu kwa ajili ya kutekeleza
miradi hiyo itakayosaidia kukuza uchumi wa nchi na kuwaondolea wananchi
wake umasikini, tunaamini tutapata fedha hizo” alisema Dkt. Nchemba.
Aidha,
Dkt. Nchemba aliishukuru China kwa misaada mbalimbali iliyochangia
kufanikisha miradi mbalimbali hapa nchini ikiwemo miundombinu ya Reli,
elimu, tehama, nishati, maji, kilimo, maendeleo ya viwanda pamoja na
afya na kwamba misaada hiyo itaendelea kutolewa ili kuiwezesha nchi
kukabiliana na umasikini na kukuza uchumi wake.
Kwa
upande wake, Naibu Waziri wa Biashara wa Jamhuri ya Watu wa China Mhe.
Qian Keming, aliahidi kuwa nchi yake itaendeleza uhusiano na ushirikiano
na Tanzania katika chanja mbalimbali za kiuchumi na kijamii ili iweze
kutimiza malengo yake ya kupiga hatua kiaendeleo na kuboresha maisha ya
watu wake.
Alisema
kuwa China itaendelea kuhamasisha uwekezaji kwa kuzishawishi kampuni
kutoka nchini humo kwenda kuwekeza Tanzania pamoja na kusaidia kutoa
fedha kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo.
Mheshimiwa
Keming alielezea kufurahishwa na kuongezeka kwa biashara kati ya
Tanzania na China, hususan katika biashara ya mazao ikiwemo zao la
muhogo na kwamba jitihada zaidi zinatakiwa ili Tanzania iweze kunufaika
na soko la China kwa kuongeza uzalishaji wa mazao ya chakula
yanayohitajika kwa wingi nchini mwake.
Mkutano
huo umewshirikisha Mawaziri kadhaa wa Kisekta Pamoja na Waziri wa Fedha
na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mhe. Dkt. Saada Salum
Mkuya, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Emmanuel Tutuba, na
maafisa kadhaa kutoka Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki.
No comments:
Post a Comment