Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab na ujumbe wake wakiwa katika mazungumzo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, Dkt. Ahmad Hassan Al-Hamadi ( wa pili kulia) katika kikao kilichofanyika katika Ofisi za Wizara hiyo Jijini Doha, Qatar tarehe 28 Agosti 2022.
Tanzania imeihakikishia Qatar kuwa ipo tayari kutoa vijana
watakaoweza kufanya kazi nchini humo, hususan katika kipindi hiki
ambacho mahitaji ya nguvukazi ni makubwa kutokana na nchi hiyo kuwa
mwenyeji wa Mashindano ya Mpira wa Miguu wa Kombe la Dunia
yatakayochezwa mwezi Novemba 2022.
Hayo yameelezwa wakati wa
mazungumzo baina ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje na
Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Fatma Rajab na Katibu Mkuu wa
Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, Dkt. Ahmad Hassan Al-Hamadi
yaliyofanyika kwenye Ofisi za Wizara hiyo Jijini Doha, Qatar tarehe 28
Agosti 2022.
Mazungumzo hayo yamefanyika ikiwa ni moja ya utekelezaji wa Mkataba wa Kazi uliosainiwa kati ya Tanzania na Qatar mwaka 2014.
“Tunawapongeza
Qatar kuwa mwenyeji wa Kombe la Dunia la FIFA litakaloanza mwezi
Novemba mwaka huu. Aidha, napenda kukufahamisha kuwa Tanzania imewaandaa
vijana wake wenye ujuzi na hivyo tunaomba kupata nafasi za ajira na za
viza (visa allocation) kwa ajili ya Watanzania kuweza kuja kufanya kazi
huku hasa wakati huu wa kombe la dunia,” aliongeza Balozi Fatma.
Katika
Kikao hicho, viongozi hao pia wamesisitiza umuhimu wa kuimarisha
ushirikiano mzuri uliopo kati ya nchi hizi mbili hususan katika maeneo
ya uwekezaji na biashara. Balozi Fatma alieleza kuwa Serikali ya awamu
ya tano chini ya Rais Samia Suluhu Hassan imefanya maboresho makubwa ya
mazingira ya uwekezaji na biashara, hivyo ametoa wito kwa
wafanyabiashara wa Qatar kuja kuwekeza nchini katika maeneo mbalimbali
kama vile utalii, kilimo, madini, maliasili, uvuvi na utamaduni.
“Napenda
kukuhakikishia kuwa Tanzania inazo fursa mbalimbali za biashara na
uwekezaji na tunawakaribisha Serikali ya Qatar pamoja na wananchi wenu
kuja kuwekeza nchini hususan katika sekta za utalii, madini, biashara na
uwekezaji,” ameeleza Balozi Fatma.
Mkutano huo ulioandaliwa na
Wizara ya Mambo ya Nje ya Qatar, pia umehudhuriwa na Katibu Mkuu, Ofisi
ya Waziri Mkuu – Kazi, Vijana, Ajira na Watu Wenye Ulemavu, Prof. Jamal
Katundu, Mkurugenzi wa Idara ya Mashariki ya Kati katika Wizara ya
Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Hemed Mgaza na
Mkuu wa Utawala wa Ubalozi wa Tanzania nchini Qatar, Bi Patricia
Kiswaga.
No comments:
Post a Comment