August 11, 2022

Vyuo vya ualimu wa michezo vyaongezeka


Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Francis Michael.

 

Na Mwandishi Wetu, Tabora

SERIKALI kupitia Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia imeongeza idadi ya Vyuo vya Ualimu vinavyofundisha somo la michezo na kufanya vyuo hivyo kuwa sita kutoka vinne vilivyokuwa vinatoa mafunzo hayo awali.

Hayo yamesemwa Mkoani Tabora na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi na Teknolojia Dkt. Francis Michael  wakati akifungua Mashindano ya kitaifa ya Umoja wa Michezo ya Shule za Sekondari (UMISSETA).

Dkt Michael ameeleza kuwa hatua hiyo ni kutekeleza agizo la Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa (Mb) Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alilolitoa Mkoani Mtwara Juni 08, 2021 wakati wa Ufunguzi wa Mashindano ya UMISSETA na Agosti 04, 2022 Mkoani Tabora wakati wa ufunguzi wa UMITASHUMTA ambapo aliagiza kuwa Vyuo vyote vya Ualimu viandaliwe kufundisha somo la Michezo ili walimu watakaohitimu katika vyuo hivyo waweze kufundisha somo hilo katika shule zote za Msingi na Sekondari.
 
Ametaja Vyuo Vyuo vya ualimu vinavyofundisha somo la michezo kwa sasa kuwa ni Ilonga, Butimba, Mpwapwa,Tarime, Tabora na Mtwara Kawaida na kwamba Mpango wa Serikali ni kuwezesha vyuo vyote vya ualimu nchini kutoa elimu ujuzi ikiwemo Michezo na sanaa ili kuandaa walimu wenye stadi na ujuzi.

“Zaidi ya michezo pia tutatoa ujuzi wa kilimo, ufugaji na ufundi. Nitoe wito kwa vyuo vya ualimu nchini kujipanga katika utekelezaji huo,” amesema Katibu Mkuu Michael

Aliongeza kuwa kwa sasa Wizara iko kwenye mapitio ya mitaala ya elimu na Sera ya Elimu na Mafunzo ya Mwaka 2014 lengo ni kuhakikisha kunakuwa na mitaala itakayomuandaa muhitimu kupata maarifa, ujuzi na stadi ili kuweza kujiajiri na kuajirika na kwamba wale wenye vipaji vya michezo waweze kuandaliwa mazingira wezeshi kumudu stadi hizo iliwaweze kupata ajira kupitia vipaji hivyo.


Pia Wizara inapitia mapendekezo ya TAHASUSI za Kidato cha Tano na Sita zinazojumuisha masomo ya Sanaa na Michezo ili wanafunzi waweze kuendeleza Stadi zao walizozipata walipojifunza somo la Elimu kwa Michezo walipokuwa kidato cha Kwanza hadi cha Nne.

Akizungumzia mashindano ya UMISSETA kwa mwaka 2022 Katibu Mkuu Michael amesema imejumuisha michezo ya Mpira wa Miguu wanawake na wanaume, Netiboli, Mpira wa Kikapu wanawake na wanaume, Mpira wa Wavu wanawake na wanaume, Mpira wa Mikono wanawake na wanaume, Riadha wanawake na wanaume, Mpira wa Meza wanawake na wanaume.

Mingine ni Sanaa za Maonesho ambazo ni Ngoma, Kwaya na Mziki wa Kizazi Kipya kwa wanawake na wanaume ambapo jumla ya wanamichezo 4200 wakiwemo wanafunzi na viongozi watashiriki kwenye mashindano haya.

No comments:

Post a Comment

Pages