August 01, 2022

Waziri Dk. Gwajima aelezea Vipaumbele katika Utekelezaji wa Bajeti ya Wizara Mwaka wa Fedha 2022/23

 

 

Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima.


Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam

Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum kwa Mwaka wa Fedha 2022/23 imesema kuwa imetenga kiasi cha Sh Bilioni 45 kwa Kundi wafanyabishara ndogondogo maarufu kama Wamachinga kwa ajili ya kuendeleza ujenzi wa miundombinu katika masoko na kuwawezesha kupata mitaji ya kuendeleza biashara zao.

Hayo yamesemwa leo jijini humo na Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum Dkt. Dorothy Gwajima wakati akifafanua mbele ya wanahabari majukumu ya Wizara na utekelezaji wa Bajeti kwa mwaka wa fedha 2022/2023.

Amebainisha kuwa utekelezaji wa mpango huo unafanyika kwa Ushirikiano baina ya Wizara za kisekta zikiwemo; Ofisi ya Makamu wa Rais; Ofisi ya Waziri Mkuu; Wizara ya Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalum; OR-TAMISEMI; Uwekezaji, Viwanda na Biashara; Fedha na Mipango; Mambo ya Ndani ya Nchi; OR-Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora na Wizara ya Ardhi na Maendeleo ya Makazi.

Amesisitiza kuwa kuhusu maendeleo ya Vyuo vya Maendeleo ya Jamii, Wizara imetenga Tsh. 5,300,000,000/= kwa ajili ya kuboresha mazingira ya kujifunzia na kufundishia katika Taasisi ya Maendeleo ya Jamii Tengeru na Vyuo nane vya Maendeleo ya Jamii.

“Fedha hiyo itatumika kuendelea kujenga na kukarabati mabweni, madarasa, kumbi za mihadhara, majengo ya utawala pamoja na Maktaba”. Amesema Waziri Gwajima.
Amesema katika kuwezesha wanawake kiuchumi, Serikali itaendelea kuhamasisha wanawake kujiunga katika majukwaa ya uwezeshaji wanawake kiuchumi. Majukwaa haya yapo kuanzia ngazi ya Kijiji/Mtaa, Kata, Halmashauri, Mkoa na Ngazi ya Taifa.

“Ili kuimarisha majukwaa haya, Wizara imepanga kutumia kiasi cha Shilingi 15,940,000 kusambaza Mwongozo wa Majukwaa ya Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi pamoja na kuzindua Jukwaa la Kitaifa la Uwezeshaji Wanawake Kiuchumi”. Amesema 

Ameongeza kuwa amesema katika kuhakikisha ahadi za nchi zinafikiwa, Serikali iko katika hatua za mwisho za kukamilisha Andiko linalolenga kuweka mazingira wezeshi ya utekelezaji wa Ahadi za Nchi kuhusu Jukwaa la Kizazi Chenye Usawa. Jumla ya Shilingi 81,200,000 imepangwa kutumika.

Ameeleza kuwa katika kuwezesha wanawake kiuchumi, Serikali itaendelea kutoa mikopo yenye masharti nafuu kwa wanawake wajasiriamali kupitia Mfuko wa Maendeleo ya Wanawake ambapo kiasi cha Shilingi 600,000,000 zimetengwa.

“Fedha hizi ni kwa ajili ya kutoa mikopo kwa vikundi vya wanawake wajasiriamali pamoja na mwanamke mjasiriamali mmoja mmoja”. Ameeleza Waziri Gwajima 

Pia amesema kuwa Serikali itaendelea kuratibu afua za kukuza usawa wa kijinsia na kutokomeza ukatili dhidi ya wanawake. Mwanamke ndiyo mlezi wa familia na jamii kwa ujumla, hivyo anahitaji kulindwa dhidi ya vitendo vya ukatili. Katika eneo hili, Wizara imetenga kiasi cha Shilingi 168,980,000.

No comments:

Post a Comment

Pages