August 22, 2022

Wizara ya Maji Zanzibar yapongezwa

 

Naibu waziri WMNM Shaaban Ali Othman ( kulia), Mwenyekiti wa Kamati ya Mawasiliano, Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar Abdallah Rashid( kati) wakiwa katika kikao cha Majumuisho katika ukumbi wa ZURA.


Na Salma Lusangi

 

Naibu Waziri Wizara ya Maji, Nishati na Madini (WMNM) Shabaan Ali Othman amesema uongozi wa wizara yake uko tayari kukosolewa pamoja  na kupokea maelekezo yaliyotolewa na kamati ya Mawasiliano,Ardhi na Nishati ya Baraza la Wawakilishi Zanzibar, ili kuleta ufanisi katika  majukumu ya  wizara hiyo.

 

Akizungumza katika kikao cha majumuisho kilichofanyika katika ukumbi wa ZURA Maisara Zanzibar, baada ya kamati hiyo kumaliza ziara ya  kutembelea miradi ya umeme na maji kwa Unguja na Pemba ambayo  inatekelezwa na  WMNM, alisema wapo tayari kukosolewa kiutendaji  pamoja na kupokea ushauri ili kuleta ufanisi katika kuwahudumia  wananchi. 

 

“Kwanza nawapongeza watendaji wote hasa nampongeza Katibu Mkuu Kilangi, kama wizara tumepokea maelekezo ya kamati,tutayatekeleza kama tulivyotumwa naomba kamati  isisite kutukosoa  zaidi naona kamati imetoa ushauri mzuri utatusaidia sana katika kutekeleza majuku yetu, tumeyapokea maelekezo yote” alisema Othman.

 

Alisema wizara yake itaongeza kasi ya kufuatilia utekelezaji wa miradi ya Maji na Nishati pamoja na kuangalia upya mikataba ya wakandarasi kwa lengo la kumaliza miradi yote kwa wakati ili kuwaondolea shida wananchi.

 

Akizungumza Mwenyekiti wa kamati hiyo Abdallah Rashid Aballah ameitaka  WMNM kukamilisha miradi ya maji na umeme kwa wakati ili kutimiza  ahadi  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dkt Hussein Mwinyi aliyowaahidi wananchi kuwafikishia  huduma ya maji na umeme mjini na vijijini.

 

Alisema   miaka mitano sio mengi, lazima ahadi za Mhe. Rais zikamilike kabla ya kufikia muda huo kwani wananchi bado wanalalamikia ukosefu wa kupata huduma ya maji.

 

Alisema kamati yake  imeshatoa maelekezo kwa changamoto walizoziona katika  Miradi ya Maji ikiwemo kuwashirikisha  waakaazi wa eneo husika wakati wa kufanya  utafiti kabla ya kuanza  utekelezaji wa  mradi/ miradi ili kuepusha migogoro isiyonaulazima.

 

Aidha amepongeza  ripoti na utekelezaji  wa miradi inayosimamiwa na WMNM kwani kamati imeona vifaa vya miradi ya umeme ambavyo vimenunuliwa na Shirika la Umeme Zanzibar (ZECO) pamoja kuona maendeleo ya miradi ya Maji ikiwemo uchimbaji wa visima, ujenzi wa matangi na utandazaji wa mabomba ya maji kwa unguja na Pemba.

 

Mapema katibu Mkuu WMNM  Joseph Kilangi aliwasilisha ripoti ya utekezaji wa wizara hiyo kwa kipindi cha Febuari hadi June ,2022 ikiwemo mafanikio na changamoto zilizowakabili katika utekelezaji wa miradi ikiwemo idadi ya visima vilivyofanikiwa kuchimbwa, pamoja changamoto za kiutalamu, vifaa vya miradi kuchelewa kufika kwa wakati hali ambayo ilisababisha baadhi ya miradi kusita kidogo kiutendaji.

 

Alisema hivi sasa vifaa vingi vya miradi vimeshawasili nchini ikiwemo mita za umeme, mabomba ya maji , kokoto , saruji nk hivyo  kazi itaendelea kwa kasi zaidi kwasababu  watendaji wa wizara yake wanafanya kazi kwa mashirikiano ya karibu ili kuleta ufanisi zaidi.

 

Kwa Upande wake Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka  ya Maji Zanzibar ( ZAWA) Mhandisi Dkt Salha Mohammed Kassim alisema  wanafanya kazi kwa usimamizi mkubwa bali amekabiliwa na changamoto ya  ukosefu wa watalaam hivyo wakati mwengine anahitaji  kuazima wahandisi na mafundi kutoka Tanzania Bara ili kuongeza kasi ya utendaji.

 

“Naomba Serikali kuekeza nguvu ya elimu kwa vijina katika fani ya Mechanical engineer, Civil engineer na Electrical engineer  kwani wakati mwengine huwa na lazimika kuomba  wataalamu kutoka Tanzania bara kwasababu nimetafuta hapa Zanzibar nimekosa” alisema Mhandisi Dkt Salha.

No comments:

Post a Comment

Pages