September 16, 2022

BRELA yakutana na Wadau Taasisi za Sekta za Umma kupokea maoni Mabadiliko ya Sheria ya Leseni za Biashara ya mwaka 1972

Mkurugenzi wa Leseni kutoka Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni ( BRELA), Andrew Mkapa, akizungumza wakati alipokuwa akifungua kikao kati ya BRELA na Taasisi za Sekta za Umma.

 

Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam

 

WAKALA wa Usajili wa Biashara na Leseni (BRELA) umekutana na wadau wa Taasisi za Sekta za Umma ili kupata maoni na mapendekezo ya mabadiliko ya Sheria ya Leseni za Biashara Sura 208 ya mwaka 1972.


Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam, wakati wa kikako hicho Mkurugenzi wa Leseni kutoka BRELA, Andrew Mkapa amesema maoni hayo yatafanyika kwa siku tatu.


Amebainisha kuwa wameanza kwa kukutana na wadau kutoka taasisi mbalimbali za Serikali na kwamba siku ya pili watakutana na watu wa Sekta Binafsi huku keshokutwa ikiwa ni siku ya majumuisho ya maoni hayo kwa ajili ya kupelekwa kwa Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara kwa hatua nyingine.


“Nadhani wote mnafahamu kuna suala la leseni ya biashara ambapo wafanyabiashara wanapofanya biashara ni lazima wawe na leseni za biashara. Utoaji wa leseni ya Biashara unasimamiwa na Sheria ya Leseni ya Biashara sura 208,” amesema Mkapa na kuongeza,


“Kwahiyo BRELA ikiwa kama moja wapo ya mamlaka inayotoa hiyo leseni ya biashara, ilifanya mchakato wa kuwasiliana na Wizara Mama Wizara ya Uwekezaji Viwanda na Biashara ambayo Waziri wake ndiyo mwenya dhamana mama ya kusimamia Sheria hii, kwa ajili ya kufanya mabadiliko mbalimbali kwenye Sheria hii ili kuendana na wakati na mabadiliko yanayotokea,”.


Amesema kuwa sheria hiyo kama ilivyosheria kwa Sheria nyingine za nchi haitakiwi kuwa mgando inatakiwa kwenda na mabadiliko ya kisiasa, kiuchumi na kijamii yanayoendelea duniani na hapa nchini.


“Katika kufanya utekelezaji wa mabadidiko hayo, Wizara ya Viwanda na uwekezaji iliunda kikosi kazi ambacho kilikaa na kukusanya mapendekezo ya awali kwa ajili ya marekebisho ya sheria hii na baada ya kuwasilisha mapendekezo hayo Waziri Mwenye dhamana na Masuala ya Biashara aliagiza kwamba anataka kupata maoni ya wadau ambao kwa namna moja ama nyingine wanaitumia hii sheria,”.


Mkapa amefafanua kuwa kikao ambacho BRELA imekiandaa ni agizo la Waziri wa Uwekezaji na Viwanda na Biashara ili kuweza kupata maoni ya wadau ili kupata mapendekezo kwa ajili ya maboresho ya Sheria hiyo.


Kwa upande wake, Afisa Biashara kutoka wizara hiyo, Denis Mzamiru amesema kinachowasukuma kukusanya maoni na mapendekezo ya maboresho na marekebisho ni kuifanya sheria hiyo iendane na mazingira ya sasa ya ufanyaji wa biashara ikiendana sambamba na uwepo wa urahisi na wepesi wa wafanyabiashara kupata leseni za biashara.  


No comments:

Post a Comment

Pages