September 23, 2022

CAJ yapata Rais mpya, yapitisha Nairobi kuwa makao makuu

 

Rais wa CAJ Christopher Isiguzo.

 

Na Mwandishi Wetu, Nairobi 


BARAZA la Waandishi wa Habari Afrika, (CAJ), limefanikiwa kupata Rais wake Christopher Isiguzo kutoka nchini Nigeria, huku likitangazwa rasmi kuwa jiji la Nairobi nchini Kenya ndio yatakuwa makao makuu yake.

Maamuzi hayo yamefikiwa na bodi ya uongozi ya CAJ ilokutana juzi jumatano (Sept.21) kujadili maendeleo ya taasisi hiyo na kutoa mamlaka ya kisheria kuanzishwa kwa Sekretarieti ya CAJ Jijini Nairobi, nchini Kenya.

CAJ iliyozinduliwa Juni 23 mwaka 2020, tayari imesajiliwa rasmi chini ya sheria za Kenya ambapo katika kikao chake, bodi hiyo pia imetangaza maendeleo mapya yaliyofikiwa kisheria yanayotoa msukumo kukabiliana na changamoto za waandishi wa habari barani Afrika.

Baraza la CAJ linalenga kuleta mtazamo wa Kiafrika kwa masuala ya kushughulikia changamoto za uhuru wa vyombo vya habari, usalama wa wanahabari na upatikanaji wa habari, unaoathiri wanahabari wanapokuwa wakifanya kazi zao kulingana na Ajenda ya Umoja wa Afrika 2063 na mwamko wa Kiafrika kukabiliana na masuala hayo.

Rais wa CAJ Isiguzo kutoka nchini Nigeria ambaye pia ni Rais wa Muungano wa Wanahabari wa Nigeria (NUJ) anabainisha kuwa Baraza hilo linaendelea kuchukua jukumu la kulinda na kutetea uhuru wa kujieleza na habari kama ilivyoainishwa katika Azimio la Kanuni za Uhuru wa Kujieleza na Kupata Habari Barani Afrika.

Isiguzo alichaguliwa kuwa Rais mpya wa CAJ kwenye mkutano wa Baraza la Uongozi, akichukua nafasi ya Rais mwanzilishi Alexandre Niyungeko, Rais wa Muungano wa wanahabari wa Burundi UBJ ambaye amejiuzulu kutokana na majukumu mengine 

Katibu wa CAJ anaendelea kuwa William Oloo kutoka chama cha Wanahabari wa Kenya(KCA) na mweka hazina, Bi. Monique Kacou kutoka nchini Ivory cost (Cote d'Iviore).

Wajumbe wengine wa Baraza la Uongozi ni Ibrahima Ndiaye kutoka nchini Senegal, Bi. Idda Francis Mushi kutoka Tanzania, Bi. Indira Correia Balde kutoka Guinea - Bissau, Syabonga Dlamini wa Swaziland, Abdalle Ahmed Mumin wa Somalia Bi. Patsy Athanase wa visiwa vye Shelisheli (Seychelles) na Emmanuel Chibwana kuroka nchini Malawi.

Mjumbe mwingine mpya anatarajiwa kutangazwa wakati wowote toka sasa kuziba nafasi ya Foster Dongozi kutoka Zimbabwe aliyefariki dunia Desemba mwaka Jana.

  "Sote tunafurahia usajili wa CAJ kwa sababu hii itaiwezesha kutekeleza jukumu lake katika kuchangia utatuzi wa changamoto zinazowakabili waandishi wa habari barani Afrika,'' Alisema Alexander Niyungeko, Rais wa CAJ aliyemaliza muda wake.

 Alisisitiza wadau mbalimbali kushirikiana na Baraza hilo kuleta maendeleo yanayokusudiwa katika tasnia ya habari kwani yatatoa nafasi ya kusonga mbele na  kutoa nafasi ya kuthibitisha mamlaka hiyo kusonga mbele kwa kasi kubwa katika kutekeleza wajibu wa kushughulikia matatizo yanayowakabili wanahabari barani Afrika.

Rais Isiguzo pia alisisitiza  dhamira kubwa ya CAJ  kukabiliana na changamoto zinazowakabili wanahabari barani ambapo tayari wameidhinisha vikao vya mashauriano vya kikanda kuhusu Mpango wa Utekelezaji wa Umoja wa Mataifa kuhusu Usalama wa Waandishi wa Habari (UNPA) unaoongozwa na UNESCO.

 "Matokeo haya yatachangia kuboreshwa kwa juhudi katika kushughulikia suala hili la usalama wa wanahabari barani Afrika" Alisema Rais huyo mpya wa CAJ.

Hivi karibuni CAJ wataweka wazi mpango wa shughuli mbalimbali  watakazofanya zikilenga kushughulikia dhamira za wanahabari barani Afrika ambapo Rais Isiguzo amewaalika washirika mbalimbali wa maendeleo na masuala ya wanahabari  kufanya nao kazi nasi kufanikisha malengo hayo.


No comments:

Post a Comment

Pages