September 19, 2022

"Kukosekana Mifumo imara inayowajenga Wanawake Kiuongozi ni tatizo Ufikiaji Usawa wa Kijinsia Nchini"- Wadau


Safia Saleh Sultan, mwanasheria kutoka kituo cha huduma za Sheria Zanzibar akiwasilisha mada ya mapungufu ya sheria Zanzibar zinazokwaza ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi.

 

IMEELEZWA kuwa kukosekana kwa mifumo imara inayowajengea wanawake misingi bora ya uongozi katika ngazi mbalimbali ndio kikwazo kikuu kinachokwamisha ufikiaji wa usawa wa kijinsia katika vyombo vya maamzi nchini.


Hayo yameelezwa na viongozi wa vyama vya siasa Kisiwani Pemba katika mkutano wa kujadili mbinu na hatua ambazo zinatakiwa kuchukuliwa na vyama hivyo ili kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi ulioandaliwa na Jumuiya ya Utetezi wa Jinsia na Mazingira Pemba (PEGAO) kwa kushirikiana na Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania, (TAMWA ZNZ), Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) kupitia mradi wa kuwawezesha wanawake katika Uongozi (SWIL) unaofadhiliwa na Ubalozi wa Norway.


Walisema bado kuna ufinyu wa elimu kwa wanawake katika kuzielewa na kutumia haki na wajibu wao wa kushika nafasi katika vyombo tofauti vya maamuzi na kupelekea nafasi nyingi kuendelea kukosa uwakilishi wao.


Saleh Nassor Juma, katibu wa Chama cha ACT WAZALENDO mkoa wa Chake Chake kichama, alishauri serikali na wadau wa elimu kuingiza somo la jinsia katika mtaala wa elimu ili kuwafundisha wanafunzi umuhimu na haki za usawa wa kijinsia katika ngazi za msingi.


“Lazima kuwepo kwa mtaala maalum wa somo la usawa wa kijinsia kwenye sikuli kuanzia ngazi za msingi, hii itasaidia kuwaandaa watoto wetu hasa wakike kukua wakitambua misingi ya uongozi kuanzia ngazi za chini kabisa,” alieleza.


Aidha katika hatua nyingine alishauri kuanzishwa kwa mfuko maalum wa kuwawezesha wanawake kumudu changamoto za kiuchumi zinazokwaza ushiriki wao kwenye kugombea nafasi za uongozi.


Alisema,“tunahitaji sasa bajeti ya nchi iweke kipengele cha mfuko wa uwezeshaji wanawake ili mfuko huo uwawezeshe kuwa na uwezo na nguvu za kwenda majimboni kupambana na wanaume kwani ukosefu wa nguvu za kiuchumi kwa wanawawake ni tatizo kubwa linalowakwamisha kutokana na vyama vingi kukosa ruzuku.”


Kwa upande wake Riziki Mgeni Juma, kutoka Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) alisema licha ya kuwepo kwa changamoto hiyo lakini bado vyama vya siasa pia vimeshindwa kuweka mipango rasmi ya kuwaandaa wanawake kushika nafasi za uongozi na badala yake vinatumia mapungufu hayo kuwakosesha haki zao.


Kutokana na hilo alishauri wanawake kubadili fikra za kusubiri nafasi maalum katika vyombo vya maamuzi na badala yake wajenge utaratibu wa kujiandaa mapema ikiwa ni pamoja na kushiriki katika shughuli za kijamii kwa lengo la kujiongezea uaminifu ndani ya jamii.


Mapema akiwasilisha mada juu ya hali ya ushiriki wa wanawake katika vyombo vya maamuzi, mratibu wa TAMWA Zanzibar ofisi ya Pemba, Fat-hiya Mussa, alitaja miongoni mwa changamoto ambazo zimebainika kukwaza ushiriki wa wanawake ni wanawake wasomi kutojiingiza katika siasa kwa hofu ya kupoteza nafasi zao.


Alieleza,“wanawake wengi wasomi wanaogopa kuingia katika vyama vya siasa hasa vyama vya upinzani kwa hofu ya kuogopa kupoteza ajira zao, na hii inatokana na kuwepo kwa baadhi ya sheria ambazo zinakwaza haki za wanawake kushiriki katika siasa.”

Aidha alieleza kuwa vyama vya siasa kuwaandaa wanawake kuwa viongozi bado ni changamoto kwa vyama vingi nchini na kupelekea idadi ya wanawake wanaojitokeza kugombea nafasi hizo kuwa ndogo katika ngazi mbalimbali. 

 

“Katika uchaguzi wa mwaka 2020, jumla ya wanawake 216 kati ya wanaume 939 sawa na asilimia 20% walipitishwa na vyama vyao kuwa wagombea kwa nafasi tofauti wakiwemo 61 kugombea nafasi za Wawakilishi, 74 Madiwani, 81 kwa nafasi za Ubunge. Walioshinda mchakato huu ni 37 tu,” alieleza mratibu huyo.


Kwa upande wake Safia Saleh Sultan, mwanasheria kutoka kituo cha Huduma za Sheria Zanzibar alisema kukosekana kwa mifumo imara ni pamoja na uwepo wa sharia ambazo zinakwaza usawa wa kijinsia katika vyombo vya maamuzi.


Alifahamisha, “Sheria ya uchaguzi na. 4 ya 2018, ambapo licha ya kwamba Sheria hii inasimamia na kutoa muongozo mzuri wa jinsi ya kupatikana kwa wagombea na viongozi wa nchi lakini bado ipo kimya katika kueleza utaratibu wa kupatikana kwa wagombea katika hatua za awali kupitia vyama vyao hasa ikizingatiwa kila chama kuwa na utaratibu wake wa upatikanaji wa wagombea.  Hivyo ni vyema Sheria hii ikaweka utaratibu rasmi wa kulazimisha upatikanaji wa wagombea wa kila chama kwa kuzingatia usawa wa kijinsia katika kila nafasi.”


Mkutano huo wa vyama vya siasa uliolenga kujadili mbinu na hatua za kuchukuliwa na vyama vya siasa kuongeza ushiriki wa wanawake katika nafasi za uongozi ni mwendelezo wa utekelezaji mradi wa kuwawezesha wanawake katika Uongozi (SWIL) ambao unatekelezwa kwa mashirikiano ya Chama cha Wandishi wa Habari Wanawake Tanzania, (TAMWA ZNZ) Jumuiya ya Wanasheria Wanawake Zanzibar (ZAFELA) pamoja na  Jumuiya ya Utetezi wa Jinsia na Mazingira Pemba (PEGAO) kwa kufadhiliwa na Ubalozi wa Norway.

No comments:

Post a Comment

Pages