Dotto Mwaibale na
Philemon Mazala , Singida
WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu
Profesa Joyce Ndalichako amekagua mradi wa Kitalu Nyumba wa kilimo cha mbogamboga na matunda wenye
thamani ya Sh. 30 Milioni unaotekelezwa Manispaa ya Singiga.
Akikagua mradi huo leo Septemba 17, 2022 alisema ameridhishwa na
utekelezaji wake na kueleza kwamba Manispaa ya Singida ni miongoni mwa wilaya zilizofanya vizuri kati ya wilaya
117.
Ndalichako alisema mradi huo unafadhiliwa na ofisi ya Waziri Mkuu kwa
maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan ambaye alielekeza kubuniwa kwa miradi
itakayoweza kuwakomboa vijana kiuchumi na kuwapa ujuzi.
"Miradi ya namna hii inatekelezwa katika mikoa 17 ambapo pia
tumezifikia halmashauri za wilaya 117 na vijana takribani 12,000 wamenufaika na
mafunzo ya mradi huu wa kitalu nyumba na fedha ambazo zimetumika kwa ajili ya
mafunzo hayo ni Sh. 5.3 Bilioni" alisema Ndalichako.
Ndalichako alisema vijana wamekuwa wakifurahia mradi huo na kuwa
wataendelea kumpigia hodi Rais Samia Suluhu Hassan ili aendelee kusaidia mradi
huo wa kuwawezesha vijana.
Aidha Ndalichako alisema programu ya kuwajengea ujuzi vijana kwa mwaka
2022/ 2023 Serikali imetenga Sh. 9 Bilioni na katika mafunzo wanayotegemea
kuyafanya ni maeneo maalumu ambayo wanafuga samaki kama kule Ziwa Victoria.
Alisema katika mwaka huu wa fedha wanatarajia kujenga vituo Atamizi vitano
ambavyo vitakuwa na vifaa vya usindikaji na uchakataji wa mazao mbalimbali na
kupitia mfuko wa maendeleo ya vijana wanapewa fursa ya kuomba mkopo ili
kuongeza thamani ya mazao hayo na Serikali itapitia maombi hayo kuona kama
yatakidhi vigezo.
Ndalichako alisema kumekuwa na tabia ya vijana kushindwa kurejesha mikopo
ya asilimia 10 wanayopewa na halmashauri hivyo kutokana na hali hiyo hivi sasa
wamependekeza wawe wanakopeshwa vifaa kulingana na mahitaji yao na baadaye
kurejesha mkopo huo.
"Nina waagiza wakuu wa wilaya, wakurugenzi kuhakikisha wanatoa mikopo
hiyo kwa vijana kwani ni maelekezo ya Rais Samia Suluhu Hassan na kila robo ya
mwaka mnatakiwa kufanya hivyo" alisema Ndalichako.
Alisema kwa mwaka huu wa fedha 2022/ 2023 kupitia mfuko wa Waziri Mkuu
zimetengwa Sh.Bilioni 1 kwa ajili ya kuwakopesha vijana hivyo wametakiwa
kuchangamkia fursa hiyo.
Akizungumzia kuhusu mkopo wa asilimia 10 alisema zamani ulikuwa ukitolewa
kwa vikundi lakini hivi sasa wameweka uratibu wa kumpa mtu yeyote ambaye
atakuwa na sifa kulingana na jambo analotaka kulifanya baada ya kulifanyia
ubunifu.
Mratibu wa mradi huo Manispaa ya Singida, Simon Magige alisema walipokea
vifaa vya ujenzi wa kitalu nyumba na fedha za kuendesha mafunzo vyote vikiwa na
thamani ya Sh. 30 Milioni.
Alisema jumla ya vijana 100 wamenufaika na mradi huo 20 kati yao wakipata mafunzo ya utengenezaji wa kitalu nyumba huko 80 wakiwa wamepata mafunzo ya uzalishaji wa mbogamboga kwa kutumia teknolojia ya kitalu nyumba kibiashara (Kilimo Biashara).
No comments:
Post a Comment