September 30, 2022

RIPOTI : IDADI YA MAPATO YA WATALII NCHINI YAZIDI KUONGEZEKA


 Mwenyekiti wa Kamati ya Ripoti ya  Utafiti wa Watalii ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Juma S. Mkomi akisoma   ripoti ya Matokeo ya Utafiti wa Watalii Walioondoka nchini mwaka 2021 mara baada ya uzinduzi wa ripoti hiyo iliyotolewa leo Ijumaa Septemba 30, 2022 Jijini Arusha.
 
 
Na Mwandishi Wetu


Idadi ya mapato yatokanayo na utalii imeongezeka  kutoka Dola za Kimarekani milioni 714.59  kwa mwaka 2020  hadi kufikia Dola za Kimarekani milioni 1,310.34 kwa mwaka  2021 

Taarifa hiyo imetolewa leo Ijumaa Septemba 30, 2022 Jijini Arusha  na Mwenyekiti wa Kamati ya Ripoti ya  Utafiti wa Watalii ambaye ni Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Juma S. Mkomi wakati wa uzinduzi wa ripoti ya Matokeo ya Utafiti wa Watalii Walioondoka nchini mwaka 2021.

Naibu Katibu Mkuu  Mkomi amesema taarifa ya utafiti huo inaonesha kuwa Tanzania inazidi kufanya vizuri katika sekta ya utalii huku mapato yatokanayo na utalii  yakiongezeka mwaka hadi mwaka.

Amesema mwaka mmoja baada ya mlipuko wa janga la UVIKO-19,  idadi ya watalii  iliongezeka kutoka watalii 620,867 mwaka 2020 hadi kufikia watalii 922,692 mwaka 2021 ambalo ni sawa na ongezeko la asilimia 48.6 

Amezitaja sababu zilizochangia  ongezeko la watalii hapa nchini mara baada ya mlipuko wa Janga la UVIKO 19 kuwa ni  jitihada zinazofanywa na Serikali pamoja na Sekta binafsi katika kutangaza vivutio vya utalii ndani na nje ya nchi

Mkomi  amesema, matokeo ya utafiti yanaonesha idadi kubwa ya watalii walikuja hapa nchini kwa ajili ya  kutembelea hifadhi za wanyamapori na fukwe.

Utafiti huo umefanywa na Wizara ya Maliasili na Utalii kwa kushirikiana na Benki Kuu Tanzania (BOT), Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS),  Idara ya Uhamiaji, Kamisheni ya Utalii Zanzibar na Shirikisho la wawekezaji katika Sekta ya Utalii Zanzibar ( ZATI)

Mkomi  amesema  takwinu za utafiti huo,  zimepatikana kutokana na utafiti uliofanywa  katika vituo vikubwa nane vya watalii, ikiwemo viwanja vya ndege  vya kimataifa pamoja na maeneo ya njia za  kuingilia na kutokea watalii.

Matokeo ya utafiti huo yameonesha kuwa idadi kubwa ya watalii wametokea nchi ya Ufaransa ikifuatiwa  na  Marekani,  Kenya  pamoja na Zambia 


Katika hatua nyingine, Naibu Katibu Mkuu Mkomi amesema matokeo ya  utafiti huo yameonesha kuwa wastani wa matumizi ya mtalii kwa siku hapa nchini yaliongezeka kutoka dola za  Kimarekani 152 mwaka 2020 hadi kufikia dola za Kimarekani 199 mwaka 2021

Naye, Kaimu Mkurugenzi wa Utalii  Wizara ya Maliasili na Utalii, Richie Wandwi amesema  kwa sasa Wizara ya Maliasili na Utalii imejidhatiti kuwekeza nguvu katika utalii wa fukwe kwa vile ni aina ya utalii ambao unaonekana kupendwa na watalii  wengi wanaoingia nchini.

Ameongeza kuwa, Wizara itaendelea kuzifanyia kazi changamoto mbalimbali ambazo baadhi ya watalii wamekutana nazo ili kuhakikisha idadi ya watalii inazidi kuongezeka na vivutio vilivyopo hapa nchini vinatangazwa kwa kasi zaidi katika  Jumuia za Kimataifa.

Utalii ni miongoni mwa sekta muhimu katika uchumi wa dunia ambapo  idadi ya watalii duniani iliongezeka kwa takribani asilimia tano na kuchangia asilimia 6.8 ya mauzo ya nje, na kuzalisha ajira milioni 333.

No comments:

Post a Comment

Pages