September 30, 2022

TRC lazindua Mafunzo kwa Watendaji Watakaosimamia Uendeshaji SGR


Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Reli Tanzania (TRC), Masanja Kadogosa akizungumza jijini Dar es Salaam katika Uzinduzi wa Mafunzo ya Vitendo kwa Watendaji watakaosimamia Uendeshaji wa Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR).

 

Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam


Shirika la Reli Tanzania (TRC) limezindua Mafunzo kwa Vitendo kwa Watendaji wake yatakayotolewa na Wataalamu 15 kutoka Shirika la Reli la Korea Kusini (KORAIL) kwa muda wa miaka mitatu lengo likiwa kubadilishana uzoefu na kuwajengea uwezo  wafanyakazi watakaoshiriki uendeshaji Mradi wa Reli ya Kisasa (SGR) utakapoanza kutoa huduma rasmi mwezi Februari, 2023.

Hayo yamesemwa leo jijini humo na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika hilo Masanja Kadogosa na kwamba  mafunzo hayo ni utekelezaji wa mkataba wa mafunzo kwa vitendo uliosainiwa Julai mwaka na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassani Ikulu Jijini Dar es Salaaam kati ya TRC na KORAIL.


Amebainisha kuwa maandalizi ya uendeshaji wa treni hiyo yanaendelea vizuri kwani miundombinu ya kipande cha kwanza kinachotoka Dar es Salaam hadi Morogoro kimekamilika kwa zaidi ya asilimia 97 huku kipande cha pili kutoka Morogoro hadi Makutupora kimeshakamilika zaidi ya asilimia 91.

“Haya ni maandalizi ya uendeshaji wa treni ya kisasa ambayo miundombinu yake kwa kipande cha kwanza cha Dar es Salaam hadi Morogoro imekamilika kwa zaidi ya asilimia 97 na kipande cha pili kutoka Morogoro hadi Makutopora kimekamilika kwa zaidi ya asilima 91” amesema Kadogosa.

Amesisitiza kuwa TRC limeamua kuwatumia wataalamu  KORAIL kutoa mafunzo hayo kwa watendaji wa TRC kwasababu uendeshaji wa treni ya kisasa Korea ya Kusini ni salama kwa asilimia 99.9 ambapo inaonesha wana wataalamu waliobobea katika nyanja zote za uendeshaji wa treni ya kisasa.

Amezitaja baadhi ya nyanja ambazo wataalamu wa KORAIL watatoa mafunzo ya nadharia na vitendo ni jinsi ya kupanga treni, uongozaji wa treni, uendeshaji wa treni, biashara ya treni, kutoa utaalamu wa karakana ziweje na usafirishaji katika uendeshaji wa treni, na kwamba yatakuwa ni ya kina na yatatolewa kwa muda wa miaka mitatu.

“Ili kupata elimu nje ya muda wa kazi ni vyema kuwa na uhusiano mzuri na wataalamu hawa kutoka KORAIL kwa sababu watakuwa TRC kwa muda mrefu” amesisitiza Kadogosa.

Amefafanua kuwa uendeshaji wa treni ya kisasa utaanza rasmi mwezi Februari mwakani baada ya taratibu zote za majaribio kufanyika na kukubaliana gharama za usafirishaji na Mamlaka ya Udhibiti Usafiri wa Ardhini( LATRA).

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi kutoka KORAIL, Lee Seung Young ameushukuru Uongozi wa TRC kwa kuwaamini kwa kazi ya utaoaji mafunzo kwa vitendo katika uendeshaji wa treni ya kisasa na kuahidi kutoa mafunzo kwa ufanisi kwasababu wamekuja na wataalamu katika nyanja mbalimbali na wana uzoefu wa kutosha kwenye uendeshaji wa treni ya kisasa.

Mafunzo kwa vitendo kwa uendeshaji wa treni ya kisasa yatashirikisha watendaji vijana zaidi ya 30 kutoka TRC na wataalamu 15 kutoka KORAIL.

 

No comments:

Post a Comment

Pages