September 30, 2022

Wadau waiunga mkono serikali maadhimisho ya siku ya kichaa cha mbwa duniani

 



Na Mwandishi Wetu

KICHAA cha mbwa ni ugonjwa unaosababishwa na virusi vya kichaa cha mbwa na huathiri wanyama wote hususan mbwa na binadamu. Ugonjwa huu hauna tiba bali unakingwa kwa chanjo na kuzingatia ufugaji bora wa mbwa.

Siku ya kichaa cha mbwa duniani, huadhimishwa si ya tarehe 28 Septemba ikiwa ni kumbukumbu ya siku aliyofariki mgunduzi wa chanjo ya ugonjwa huo.

Nchi ya Tanzania kupitia serikali na wadau mbalimbali wa ustawi wa Wanyama, hushiriki pia katika kuadhimisha sikukuu hii kwa kutekeleza uchanjwaji wa mbwa katika maeneo mbalimbali nchini Tanzania.

Kauli mbiu iliyoongoza maadhimisho haya duniani kote mwaka huu inasema kichaa cha mbwa, afya moja, vifo sifuri.

Wadau wa ustawi wa Wanyama Shirika lisilo la kiserikali linalojihusisha na ustawi wa Wanyama nchini Tanzania linalojulikana kama Education for African Animals Welfare (EAAW) na Meru animals Welfare (MAWO) hawakuwa nyuma katika kuiunga serikali mkono katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa kichaa cha mbwa, mbali na kuwa sehemu ya shughuli zao, lakini pia kuadhimisha siku hii muhimu katika kuikomboa jamii yetu dhidi ya maangamizi yatokanayo na kichaa cha mbwa.


Akizungumza kwa niaba ya wadau hao, Mkurugenzi  wa EAAW Bw. Ayubu Nnko amesema kuwa kwa muda mrefu wamekuwa wakishirikiana na Wilaya ya Mkalama Mkoani Singida kwa kutoa chanjo ya kichaa cha mbwa Pamoja na matibabu, huku MAWO wakihudumia Wilaya ya Simanjiro mkoani Manyara.


Bw. Nnko ameeleza kuwa mwaka huu walizindua maadhimisho hayo siku ya tarehe 23 Septemba katika Kijiji cha Yulansoni na Msingi kata ya Kinyangiri Wilaya ya Mkalama, ambapo mpaka sasa zaidi ya Mbwa 518 na Paka 29 wamekwishakupatiwa chanjo na zoezi hilo litaendelea hadi tarehe 2 Octoba ambapo wanategemea wanategemea kuhusisha vijiji vya Nduguti na Maziliga.


Kwa upande wa Simanjiro, MAWO wameweza kuendesha zoezi hilo katika vijiji vya Naisinya, Naepo,Mererani, Shambarai na Orkesmet.


Akizungumza katika uzinduzi wa maadhimisho hayo katika Wilaya ya Mkalama Kijiji cha Yulansoni, Daktari wa mifugo wilaya ya Mkalama Elias Mbwambo amelishukuru  EAAW na kusema kuwa shirika hilo limekuwa mstari wa mbele kushirikiana na Wilaya ya Mkalama bega kwa bega katika mapambano dhidi ya kichaa cha mbwa na kuitaka jamii kutoa ushirikiano pale wanapoletewa chanjo na kuhakikisha wanashiriki ipasavyo katika matunzo ya mbwa na paka ili kuepusha madhara.


Kwa upande mwingine Mbwambo ameeleza kuwa Mbwa wamekuwa wakifugwa na binadamu tangu ustaarabu ulipoanza na wanafugwa kwa malengo mbalimbali yakiwemo ulinzi, kuchunga mifugo, uwindaji, n.k. Zaidi ya asilimia 98 ya mbwa wanaofugwa nchini ni wa asili (mongrel) na mbwa wachache ni wa kisasa ambao hufugwa zaidi maeneo ya mjini.


Amesisitiza kuwa Mbwa kama mifugo wengine wanatakiwa kupatiwa huduma zote za msingi kama chakula, maji, matibabu, malazi na kuogeshwa kwenye dawa za kuua wadudu. Kulingana na Sheria za Tanzania, mbwa hatakiwi kuachwa akitembea mitaani.


Halikadhalika amewatahadharisha wafugaji kuhakikisha kuwa, mbwa wanafungwa kwenye banda au mnyororo muda wote wa mchana. Kwa mbwa wanaotumika kwa kazi za kuchunga mifugo au kuwinda, ni vema wakawa chini ya uangalizi wa mwenye mbwa ili wasidhuru watu wengine;
Pia ni vyema mbwa akapata mafunzo ya msingi ili aweze kutii amri ya anaemmiliki ili kuepusha madhara
Ni Dhahiri kuwa kuna madhara mbalimbali yanayotokana na kutokuzingatia ufugaji bora wa mbwa. 

Madhara hayo ni Pamoja na Kung`ata na kujeruhi watu au mifugo mingine hivyo kupata kesi. Kusababisha hofu na kuwa tishio kwa jamii, Kueneza magonjwa kama vile kichaa cha mbwa na tegu wa mbwa.


Kichaa cha mbwa huambiza kwa njia ya kung’atwa na mbwa mwenye ugonjwa huo. Binadamu pia anaweza kuambukizwa kwa kugusa mate ya mbwa mwenye kichaa.


Dalili za ugonjwa wa kichaa cha mbwa ni Pamoja na Mbwa kubadilika tabia, ama kuwa mkali au mpole kuliko ilivyo kawaida. Mbwa kushindwa kula, kukwepa maji na kupooza miguu ya nyuma. Kdondosha mate mengi na ulimi kuning’inia nje ya mdomo. Kubweka mara kwa mara wakitoa mlio usio wa kawaida.

Akihitimisha Mkurugenzi wa EAAW amesema kuwa kuna umuhimu mkubwa jamii hasa kwa maeneo ya vijijini kushirikishwa kwa kiasi kikubwa katika tafiti na uenezwaji wa elimu juu ya matunzo ya Wanyama, kwani kwa kufanya hivyo itakuwa rahisi kwa serikali na wadau mbalimbali kutatua matatizo yanayowakabili wananchi na sekta ya mifugo.

Hali kadhalika, amevitaka vyombo vya Habari kushiriki zaidi katika kutangaza shughuli zinazofanywa na serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali kuendeleza sekta ya mifugo, ustawi wa Wanyama na jamii kwa ujumla.

Kilele cha maadhimisho ya kichaa cha mbwa huadhimishwa kila Septemba 28 ya mwaka duniani kote.

No comments:

Post a Comment

Pages