Na Mwandishi Wetu
WACHIMBAJI madini wa Umoja wa Kwahemu wa Kijiji cha Yobo, Kitongoji cha Yobo Kata ya Anet iliyopo Chamwino Dodoma wamemuomba Rais Samia Suluhu Hassan awapatie eneo la kuchimba madini ili waweze kujikwamua kiuchumi na kuiingizia serikali mapato.
Ombi hilo limetolewa hivi karibuni na Mwenyekiti wa wachimbaji hao, Hussein Kimolo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari hii kwa niaba ya wananchi 300 waliounda umoja wa vikundi 14 vya wachimbaji.
Kimolo alisema wameamua kumuomba rais kwa kuwa ni kiongozi mkuu wa taifa letu na ni mama anayeelewa changamoto zinazowakabili wananchi hususan wa kipato cha chini.
Mwenyekiti huyo aliongeza kuwa, tayari wameanza kuchimba madini kwenye eneo lisilo na tija walilopewa na wizara ya madini.
Alisema, baada ya kuona hawanufaiki kiuchumi zaidi ya pesa wanazopata kuishia kulipa mapato ya serikali walipeleka ombi kwa viongozi wa madini na wakuu wa mkoa wa Dodoma waliopita kabla ya huyu wa sasa, Rosemary Senyamule ili wapewe viwanja vitatu vyenye tija kwenye eneo linalomilikiwa na Kampuni ya Ruvu Gemstone Mining inayomilikiwa na mzungu raia wa Ugiriki aitwaye Milcan Dimist bila mafanikio.
Akielezea kwa undani sababu iliyowafanya wamuombe Mama Samia awepe eneo hilo la kuchimba madini, Kimolo alisema.
“Shughuli ya uchimbaji tunaifanya baada ya kukata leseni za kuchimba madini aina ya nikeli kwenye viwanja vitano kati ya tisa ambavyo mzungu Dimist anavimiliki alivyovikatia leseni nane zenye ukubwa usiopungua hekta 6 kwa kila leseni.
Aliongeza kuwa waliomba viwanja hivyo vitano na kukata leseni kufuatia mzungu huyo tangu aliporithi viwanja hivyo kwa baba yake ambaye ni marehemu zaidi ya miaka 33 iliyopita kushindwa kuchimba kwenye viwanja vyote isipokuwa kimoja tu.
“Tulipobaini jinsi serikali inavyokosa mamilioni ya fedha za kodi kupitia mzungu huyo kushindwa kuchimba kwenye viwanja hivyo, tulimuomba aliyekuwa mkuu wa mkoa wa Dodoma wakati huo, Bilnith Mahenge atugawie viwanja vitano kutoka anavyomiliki mzungu huyo akatushauri tuunde vikundi na kukata leseni, tukafanya hivyo.
“Tangu tulipokata leseni hizo mwaka 2019 tumepewa viwanja viwili visivyo na tija ambavyo miaka thelathini na tatu iliyopita kampuni ya Kolea ilichimba madini na kuacha mashimo tupu,” alisema Kimolo.
Alivitaja viwanja hivyo kuwa ni namba PML 0382 D0M na namba PML 0381 ambapo hadi leo hawajapewa vitatu vilivyobaki vilivyopo eneo lenye madini hivyo kupata hasara ya kulipa mapato ya serikali bila ya kuzalisha chochote kwa upande wao.
“Kinachoshangaza ni sisi kushindwa kupewa viwanja hivyo na kuishia kwenda kwa viongozi mara kwa mara kuwalilia wasikie kilio chetu bila mafanikio wakati tunaishi Wilaya ya Chamwino ambayo ina makazi ya rais wetu ambapo ni rahisi suala letu kushughulikiwa na kupata ufumbuzi,” alisema mwenyekiti huyo.
Aliongeza kuwa, hawana nia mwekezaji huyo aporwe viwanja vyote kwani
itakuwa si kumtendea haki kwa sababu serikali inawahitaji wawekezaji.
No comments:
Post a Comment