October 07, 2022

KITUO CHA AFYA MOSHI-ARUSHA CHAKABIDHIWA MANISPAA YA MOSHI


Naibu katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Jenifa Omolo, akimkabidhi Meya wa Manispaa ya Moshi Mjini, Mhe. Mhandisi Zuberi Kidumo, nyaraka za umiliki wa kituo cha afya Moshi-Arusha katika hafla ya makabidhiano iliyofanyika mjini Moshi mkoani Kilimanjaro. Katikati ni Mganga Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro, Dkt. Jairy Khanga.



Na Saidina Msangi, WFM, Kilimanjaro

 

Serikali imekabidhi kituo cha Afya Moshi-Arusha pamoja na mali mbalimbali ikiwemo kiwanja na majengo vyenye thamani ya Shilingi bilioni 4.3 kwa Manispaa ya Moshi ili iweze kukiendeleza kwa kutoa huduma za afya kwa wananchi wa manispaa hiyo na maeneo ya jirani. 

 

Makabidhiano ya kituo hicho yamefanyika katika Manispaa ya Moshi mkoani Kilimanjaro kati ya Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Bi. Jenifa Omolo na Meya wa Manispaa ya Moshi, Mhe. Mhandisi Zuberi Kidumo.

 

Akizungumza katika hafla ya kukabidhi kituo hicho, Bi. Omolo alisema kuwa Serikali inakabidhi kituo hicho pamoja na mali zake zote kwa manispaa hiyo ili iweze kutoa huduma kwa wananchi.

 

‘’Pamoja na majengo tunakabidhi mali nyingine ikiwemo samani 352, mitambo 70 na gari moja vyenye thamani ya Sh. milioni 94.21, mali chakavu zenye thamani ya Sh. 280,000, bunduki, bakaa za benki zilizoishia Julai 2022, madai ya kodi ya pango yenye thamani ya shilingi milioni 1.2 na madai kwa taasisi za bima za afya yenye thamani ya Sh. milioni 32.4,’’alisema Bi. Omolo.

 

 

Pia ilikabidhi madeni yenye nyaraka yenye thamani ya Sh. milioni 610.3 na yasiyo na nyaraka zinazojitosheleza yenye thamani ya sh. milioni 71.9 na ufuatiliaji wa mauzo ya magari mawili yenye thamani ya Sh. milioni 2.3.

 

 

Aidha, Bi. Omolo alimtaka Mkurugenzi wa Manispaa ya Moshi kuhakikisha kuwa kituo hicho kinafanyiwa maboresho ili kirejeshewe hadhi yake ya Hospitali na kuendelea kutoa huduma kwa wananchi wa manispaa hiyo na maeneo ya Jirani.

 

 

Alimtaka Mkurugenzi huyo kufuatilia taratibu za kuhamisha umiliki kwa kumshirikisha Kamishna wa Aridhi na kufuatilia nyaraka zilizokosekana za madai ya watumishi pamoja na kuchukua hatua stahiki kwa watumishi waliyojimilikisha mali za kituo hicho kinyume na sheria.

 

 

Aidha alisisitiza kuwa jukumu la kulinda mali za Serikali ni la wote, na kuelekeza kuwa baada ya makabidhiano mali zote ziingie kwenye daftari la mali za Serikali ambalo limeboreshwa na kuliweka katika mfumo wa kielektroniki wa usimamizi wa mali za Serikali ujulikanao kama GAMIS.

 

 

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Usimamizi wa Mali za Serikali Wizara ya Fedha na Mipango Bw. Chotto Sendo, alisema kuwa uhakiki wa mali na madeni ya kituo hicho umekamilika na Serikali kwa kutambua umuhimu wa kituo hicho imeamua kikikabidhi kwa Manispaa ya Moshi ili iweze kukiendesha kuhudumia wananchi.  

 

‘’Lengo ni kutoa huduma kwa wananchi kwa hiyo Serikali imeamua kurejesha kituo hicho Serikalini kwa Manispaa ya Moshi ili wananchi waendelee kupata huduma za kiafa katika kituo hiki’’ alisema Bw. Sendo.

 

Naye Kaimu Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Ubinafsishaji, Ufuatiliaji na Tathmnini kuitoka Ofisi ya Msajili wa Hazina Bw. Abissay Ndaki, alisema kuwa hospitali hiyo imerejeshwa Serikalini kwa jina la Msajili wa Hazina wakati taratibu nyingine zikiendelea kufanyika na kuishukuru Serikali kwa kuridhia kurejesha kituo hicho kwa Manispaa ya Moshi ili kiweze kuendelea kutoa huduma kwa wananchi.

 

Naye Mbunge wa Moshi Mjini Mhe. Priscus Tarimo, ameishukuru Serikali ya awamu ya Sita chini ya Uongozi wa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha manispaa hiyo kupatiwa kituo hicho ili kuweza kutoa huduma kwa wananchi wake na kuboresha upatikanaji wa huduma za kiafya.

 

Kituo cha afya Moshi/Arusha kilianzishwa mwaka 1973 kama utekelezaji wa agizo la Serikali kwa mashirika ya Umma Na.2/46/050 la tarehe 17 Novemba, lililotaka mashirika ya Umma yanayohusika na viwanda kutoa huduma za tiba na kinga pamoja na huduma za kuzuia na kutibu madhara yanayotokana na mazingira ili kuboresha afya za wafanyakazi.

 

 

Majengo ya Kituo hicho yalijengwa kwa ufadhili wa Serikali ya Uholanzi na kituo kikikiwa na hadhi ya Hospitali huku kikitegemea michango ya wenye viwanda vilivyopo Moshi na Arusha wakati huo ili kukiendesha.

 

 

Hata hivyo miaka ya 1990 baada ya viwanda hivyo kushindwa kujiendesha kulisababisha Wizara ya Afya kuishusha Hospitali hiyo kuwa Kituo cha Afya.

No comments:

Post a Comment

Pages