October 07, 2022

NABI ATAMBA KUNASA 'FILE' LA IBENGE


Na John Marwa

KOCHA Mkuu wa klabu ya Yanga SC Nasriddine Nabi ametamba kuelekea mchezo wa mkondo wa kwanza wa Ligi ya Mabingwa Afrika CAFCL dhidi ya Al Hilal ya Sudan.



Nabi ataiongoza Yanga kesho katika mchezo wa hatua za awali kuwania kufuzu hatua ya makundi msimu huu wa 2022/2023.

Mchezo huo utapigwa katika Dimba la Benjamin Mkapa majira ya saa 16:00 kwa saa za Afrika Mashariki.

Akizungumza na wandishi wa Habari kuelekea mchezo huo Nabi amesema kikosi chake kiko tayari kuwakabili Al Hilal huku akijinadi kunasa njia za kuwaangamiza wapinzani wao.

"Ni mechi ambayo inahitaji ushindi wa jumla Ili kuweza kufuzu. Kwa upande wetu tumejiandaa kwa utulivu mkubwa sana, mashabiki wanahitaji kusikia nini tunaenda kufanya lakini tumetulia sana kwa ajili ya hii mechi"

"Tunaenda kukutana na timu nzuri, yenye rekodi nzuri kwenye michuano hii, miaka nane iliyopita niliifundisha na kuipeleka makundi,  wamekuwa bora mtawalia sasa wamekuwa wakifuzu hatua ya makundi. Al Hilal wanaifahamu Yanga na wanaiheshimu ndio maana wamecheza mechi ya kirafiki dhidi ya TP Mazembe." Amesema nankuongeza kuwa.

"Kitu ambacho ninawaambia wachezaji wangu ni kutambua kuwa tunaenda kucheza na timu nzuri na yenye uzoefu Mkubwa, hatuwezi kuwadharau kwa matokeo waliyopata katika mechi ya kirafiki kwa sababu huu ni mchezo mwingine kabisa"

"Wachezaji wako tayari kupambana kwenye mchezo wa kesho, wakijiamini kwa sababu wanamheshimu mpinzani wetu, mechi hii haitaishia kwa Mkapa bali itaenda kuishi Khatoum Sudan, ni mechi ngumu kwa sababu mshindi anaingia hatua ya makundi." Nabi ameongeza kuwa.

"Hali ambayo wachezaji waliyokuwa nayo juzi na jana inaonyesha wako tayari kupambana na Al Hilal hapo kesho, ni jambo linalonipa faraja kuwa tunaweza kupambana.

"Hii mechi ni mechi ambayo Al Hilal wamejiandaa kisawasawa, wametufatilia na sisi tumewafuatilia kujua wachezaji wao wana ubora wapi na madhaifu yao." Amesema Nabi

Licha ya mechi zao kutotaka zionyeshwe Lakini Nabi amesema amefanikiwa kutuma watu wa kuwatazama.

"Naamini namna watakavyocheza na sisi ni tofauti na walivyocheza na TP Mazembe na St George." Amesema Kocha Nabi.

Yanga watashuka kwenye mchezo huo wakihitaji matokeo zaidi ili kuvunja rekodi ya kutoshiriki hatua ya makundi kwa miaka 24.

No comments:

Post a Comment

Pages