JUKWAA
la Asasi za Kiraia (RCSF) za Ukanda wa Nchi za Maziwa Makuu Afrika
(ICGLR) limetakiwa kusimamia mambo nane ambayo yatagusa jamii ya
wananchi wa nchi 12 za jukwaa hilo.
Hayo
yamesemwa na Waziri wa Sheria na Katiba Dk Damas Ndumbaro wakati
akifungua mkutano mkuu wa tatu wa ICGRL unaofanyika jijini Dar es Salaam
kwa siku mbili kuanzia leo.
Mkutano huo mkuu wa ICGLR unatarajia kuchagua viongozi wapya ambapo kwa sasa Mwenyekiti wake ni Joseph Butiku.
Waziri
Ndumbaro amesema jambo la kwanza kwa RCSF katika Ukanda wa Maziwa Makuu
ni kusimamia amani na usalama ili kuhakikisha jamii zilizopo zinafanya
shughuli za maendeleo bila usumbufu.
"Amani
na usalama ni nguzo ya muhimu kwa jamii yoyote, sisi Tanzania
tunajivunia amani kuwepo na tutaendelea kusaidia nchi wanachama wa ICGLR
ziendelee kuwa na amani,"amesema.
Amesema jambo la pili ambalo anazitaka asasi za kiraia kusimamia ni utawala bora, sheria na demokrasia.
Dk
Ndumbaro amesema utawala bora, sheria na demokrasia sio vitu ambavyo
vinashuka kutoka angani, bali vinatengenezwa na jamii husika ambapo
asasi za kiraia ni moja wadau muhimu.
"Tatizo
la nchi za Kiafrika ni kufikiria kuwa utawala bora, sheria na
demokrasia vinapatikana kwa wazungu, hii sio kweli, lazima tutengeneze
mifumo yetu na sio kukopi, kwa mfano Chancellor wa Ujerumani anaongoza
hata miaka 17, ila sisi wananchi wakisema 10 huo ndio utaratibu wetu,
hivyo asasi zina wajibu wa kusimamia hilo," amesema.
Waziri
Ndumbaro amesema asasi za kiraia zinapaswa kuchochea maendeleo ya
kiuchumi kwa wananchi na kwamba mifumo ya kufikia huko haiwezi kuwa sawa
kwa nchi zote na kusisitiza kila nchi kutumia mifumo yake.
Waziri
huyo wa Katiba na Sheria amesema jambo la nne ni asasi hizo kupigania
utengemano wa kikanda kama Jumuiya ya Afrika Mashari (EAC), Jumuiya ya
Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC) na nyingine ambazo ni muhimu katika
kuchochea maendeleo.
"Jambo
la tano naomba mjadili uwepo wa vita na mambo yote yanayoweza
kusababisha vita na sita mjadili masuala ya kijamii katika nchi
wanachama wa ICGLR na zingine," amesema.
Dk
Ngumbaro amesema jambo la saba asasi zinapaswa kujadili mazingira
ambapo amesema Tanzania imefanikiwa katika eneo hilo kwa kuwa thelusi
moja ya nchi imetunzwa.
Amesema
jambo la nane ambalo anatamani kuona asasi za kiraia zinasimamia ni
masuala mtambuka ambayo yatahusisha makundi yote kama wanawake, vijana,
watoto na wazee ambao wanashiriki katika yote ambayo ameyataja awali.
Waziri
Ndumbaro amesema Tanzania chini ya uongozi wa Rais Samia Suluhu Hassan
itatoa ushirikiano chanya kuhakikisha hoja za asasi za kiraia
zinafanyiwa kazi.
Amesema pamoja na Serikali kushiriki kufanikisha hilo pia vyombo vya habari vinapaswa kupewa kipaumbele kwa kila hatua.
Mwenyekiti
wa RCSF katika ICGLR Joseph Butiku amesema kwa miaka takribani 18
wamekuwa wakijadili mambo ya amani, usalama, demokrasia, utawala bora,
maendeleo ya uchumi, mshikamano wa nchi wanachama, vurugu zilizozalisha
wakimbizi, mazingira na jinsia kwa ufanisi mkubwa.
Butiku
amesema wanazipongeza nchi wanachama wa ICGLR zimekuwa zikitoa
ushirikiano kwao jambo ambalo limerahisisha utekelezaji wa ajenda zao.
Mwenyekiti
huyo amesema wamekuwa wakisimamia Serikali za nchi wanachama
kuhakikisha zinatekeleza majukumu yao kwa kufuata utawala wa sheria.
"Leo
asasi za kiraia za nchi wanachama ICGLR tumekutana hapa Dar es Salaam
kujadili mambo mbalimbali ambapo pia tunarajia kesho kufanya uchaguzi
kupata viongozi wapya," amesema.
Butiku
amesema ICGLR inahusisha nchi za Afrika ya Kati, DR Congo, Tanzania,
Kenya, Uganda, Sudan, Zambia, Sudan Kusini, Burundi, Rwanda na Congo
Brazzaville ambapo kwa kiasi fulani wameweza kujenga mshikamano.
Amesema jitihada zao ni kuhakikisha mfumo wa sheria unachukua nafasi katika kuendesha nchi zote wanachama.
Naibu
Katibu Mkuu wa wa ICGLR Balozi Mohamed Yassir amesema mikakati yao ni
kuendeleza mazuri yote ambayo wamekubaliana, ili kuhakikisha nchi
wanachama zinapata maendeleo kwa kasi.
"Sisi
tumekuwa tukisimamia mipango yetu, pamoja na changamoto ambazo
zinatokea, tunaamini tutafanikiwa iwapo mshikamano wa Wadau wote utapewa
kipaumbele," amesema.
Balozi Yassir amesema katika kipindi cha janga la Uviko-19 walipitia wakati mgumu, ila wanaendelea kuimarika siku hadi siku.
Naye
Hodan Addou kutoka UN Women akiwamwakilisha Mwakilishi Maalum wa Katibu
Mkuu wa Umoja wa Mataifa, katika Ukanda wa Maziwa Makuu amesema
wataendelea kushirikiana na ICGLR ili kuhakikisha amani na usalama
unaongezeka katika ukanda huo.
Amesema
UN Women itashirikiana na ICGLR kuhakikisha kundi la wanawake linapewa
msukumo ili liweze kushiri kikamilifu katika kupigania amani na usalama.
Kwa
upande wake Dk Majaliwa Marwa kutoka UNFPA amesema watatoa ushirikiano
kwa asasi za kiraia ambazo zitakuwa zinapigania haki za raia wake kwa
kufuata misingi ya kisheria na utawala bora.
Dk
Marwa amesema UNFPA inaamini katika majadiliano ili kuweza kujenga
jamii yenye maelewano na maendeleo, hivyo wanazitaka asasi za kiraia
kusimamia eneo hilo kama inavyofanya RCSF kupitia ICGLR.
Mwenyekiti
wa Jukwaa la Asasi za Kiraia nchini Kenya Peter Ole amesema asasi za
kiraia ndio zimefanya Kenya kuwa nchi ya mfano kwa nchi nyingine hasa
mfumo wake wa uchaguzi.
Naye
Makamu Mwenyekiti wa CSO Sudan Kusini Akuoch Ajang amesema nchi yao
imepitia wakati mgumu ila kupitia ujio wa asasi za kiraia jamii inaanza
kubadilika na kutambua haki zao za msingi.
No comments:
Post a Comment