October 06, 2022

Shirika la Posta Tanzania kuzindua stempu yenye lengo la kutangaza utalii, vivutio vya nchi


Kuelekea kilele cha maadhimisho ya wiki ya posta duniani yanayotarajiwa kufanyika Oktoba 9 mwaka huu, Shirika la Posta Tanzania limeazimia kuzindua rasmi huduma mpya za kidigitali ikiwepo huduma ya posta kiganjani inayomuwezesha mteja kupata huduma mbalimbali za shirika hilo kwa njia ya simu janja yake.


Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Msemaji wa Shirika la Posta Tanzania, Elia Madulesi amesema kuwa wiki ya posta inaenda sambamba na wiki ya huduma kwa wateja hivyo shirika hilo limejipanga kikamilifu kuongeza uwajibikaji na ufanisi katika utoaji wa huduma zake.


Hata hivyo amesema katika maadhimisho hayo  yatahusisha uzinduzi wa stempu maalumu iliyotengenezwa kwa ushirikiano wa serikali za Tanzania na Oman yenye lengo la kutangaza utalii wa vivutio mbalimbali vya nchi kimatafa ili kuendelea kukuza sekta hiyo.


Amesema pia kabla ya kilele cha maadhimisho hayo yatatanguliwa na kongamano la biashara mtandao na anwani za makazi lenye lengo la kuonesha maendeleo kwenye sekta na namna ukuajiwa teknolojia unavyoweza kutumika kurahisisha maisha ya wananchi.


Amesema kongamano hilo litafanyika Oktoba 8, mwaka huu katika ukumbi wa JNICC huku wadau wakitaraj8wa kujadili mafanikio na changamoto wanazozipitia watoa huduma ya biashara mtandao.


"Miongoni mwa mada zitakazojadiliwa katika kongamano hilo ni pamoja na fursa kwa wanawake vijana katika biashara mtandao,  ubunifu katika ushindani kwenye biashara mtandao, wakulima na biashara mtandao, duka mtandao la Posta na wajasiriamali pamoja na anwani za makazi zinavyowezesha biashara mtandao," amesema


Mbali na hayo, Madulesi alisema Waziri wa Habari, Mawasiliano na Teknolojia ya Habari, Nape Nnauye anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha maadhimisho ya Umoja wa Posta Duniani (UPU) yatakayofanyika Oktoba 9, mwaka huu katika Ukumbi wa Kimataifa wa Julius Nyerere (JNICC).


Amesema katika kilele hicho kutakuwa na utoaji zawadi kwa washindi walioshinda katika mashindano mbalimbali yaliyoandaliwa kwa ajili ya maadhimisho hayo.


"Makundi yanayotarajiwa kupewa zawadi na mgeni huy rasmi ni uandishi wa barua kwa wanafunzi wa shule za msingi na sekondari wenye umri usiozidi miaka 18, uandishi wa insha wanamichezo na jamii, uandishi wa makala kwa wanahabari pamoja na wabunifu wa mifumo Tehama katika mawasiliano ya posta.


"Washindi watatangazwa mbele ya Waziri Nape na watapewa zawadi zao siku hiyo ya kilele cha maadhimisho haya ya UPU pale JNICC, pia tutashuhudia matokeo ya ushirikiano wa kibiashara nakihuduma kati ya Shirika la Posta la Tanzani na Omani ambao hivi karibuni walitiliana saini ya makubaliano hayo," amesema Madulesi


Kwa upande wake Meneja Biashara, Barua na Usafirishaji kutoka Shirika hilo la Posta, Jasson kalile amebainisha kuwa shirika la posta litaendela kujikita katika kutatua changamoto mbalimbali za kimawasiliano ndani ya jamii huku akitaja baadhi ya maeneo ya kitakii yanayotarajiwa kutangazwa kupitia stempu zao mpya kuwa ni pamoja na house of wonders(jengo la maajabu), mali kale, wanyama pori pamoja na mlima kilimanjaro.

No comments:

Post a Comment

Pages