Na Mwandishi Wetu
Kikosi cha Simba Queens kimeondoka asubui ya leo kutoka mjini Rabat Morocco kuelekea mjini Marrakech nchini humo kwa ajili ya mchezo wa mwisho wa hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Soka la Wanawake Afrika.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka ndani ya Klabu ya Simba imeeleza kuwa safari hiyo itakuwa ya masaa matatu na jioni ya leo watafanya mazoezi ya mwisho kuwakabili Green Buffalos.
"Kikosi chetu kimeondoka leo asubuhi kuelekea Marrakech ambapo mchezo wetu wa mwisho wa hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Green Buffaloes kutoka Zambia utafanyika."
"Mchezo wetu dhidi ya Green Buffaloes utapigwa Jumamosi Novemba 5, saa nne usiku kwa saa za nyumbani Tanzania."
"Safari ya kutoka Rabat mpaka Marrakech inachukua saa tatu ambapo baada ya kufika wachezaji watapumzika kabla ya kufanya mazoezi ya mwisho."
"Tunahitaji ushindi kwenye mchezo huo ili kujihakikishia nafasi ya kutinga nusu fainali ambayo ni moja ya malengo tuliyojiwekea".
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni utaratibu wa michezo ya mwisho ya hatua za makundi kuchezwa muda mmoja ambapo katika mji wa Rabat kutakuwa na mchezo wa AS Far dhidi ya Determine Girls.
Simba Queens wanashika nafasi ya tatu wakiwa na pointi tatu nyuma ya AS Far na Green Buffalos.


No comments:
Post a Comment