Ofisa Habari wa RT, Lwiza John (kulia), akizungumza na waandishi wa habari kwenye ukumbi wa Uwanja wa Uhuru jijini Dar es Salaam, kuelekea uchaguzi mdogo wa kuziba nafasi zilizo wazi. Kushoto ni Mjumbe wa Kamati ya Uchaguzi RT, Morris Okinda.
Na Tullo Chambo
FOMU za kuwania uongozi kwa nafasi zilizowazi katika Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), zimeanza kutolewa rasmi.
Uchaguzi huo unatarajiwa kufanyika jijini Dodoma Novemba 27 mwaka huu, huku nafasi zilizowazi ni Makamu wa Rais na Mjumbe wa Kamati ya Utendaji Kanda ya Pwani, ambako waliokuwa wakizishikilia walijiuzuru kutokana na sababu mbalimbali.
Akizungumza na Waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam jana, Ofisa Habari wa RT, Lwiza John, alisema fomu zimeanza kutolewa Novemba 5 (leo), na zinapatikana Ofisi za shirikisho, vyama vya riadha vya mikoa na kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.
John alisema, fomu ya umakamu wa rais itachukuliwa kwa gharama ya sh. 200,000 huku ujumbe Kanda ya Pwani ni sh. 100,000 na malipo yafanywe kupitia akaunti ya shirikisho mamba 001000210974 jina Athletics Tanzania Azania Bank.
"Mgombea atakaporudisha fomu atatakiwa kuambatanisha vivuli vya risiti ya Mali po, vyeti halisi na mgombea wa nafasi ya ujumbe aambatanishe barua toka chama cha riadha mkoa anaotokea, ikimtambulisha kama mtu anayefanya shughuli za michezo ya riadha katika mkoa huo," alisema John na kuongeza.
Mgombea anaweza kurudisha kwa kupitia barua pepe ya shirikisho tan@mf.world athletics.org au kurudisha mwenyewe ofisi za RT Taifa. Kwa atakayetuma kwa njia ya e mail atatakiwa kuja na fomu halisi na viambatanisho halisi siku ya usaili.
Ofisa habari huyo, alizitaja sifa za wagombea kuwa ni awe raia wa Tanzania na lazima awe anaishi nchini.
Awe na kiwango cha elimu kisichopungua kidato cha nne kwa ujumbe, huku umakamu rais ni kuanzia stashahada.
Sifa zingine ni awe na uzoefu wa uendeshaji mchezo wa riadha angalau miaka mitano, awe amewahi kuwa kocha, mchezaji wa riadha, mwamuzi au kushiriki katika uendeshaji wa mchezo wa riadha.
John, alizitaja sifa nyingine kuwa ni awe amehudhuria mafunzo mbalimbali ya uongozi na menejimenti inayotambuliwa nchini, pia asiwe na hatia yoyote ya kosa la jinai na kuhukumiwa kifungo jela bila uchaguzi wa faini.
Ofisa habari huyo, alisisitiza kuwa, mtu anayegombea nafasi ya Makamu wa Rais, lazima awe na uzoefu mzuri na uliothibitishwa wa angalau miaka mitano, uadilifu, haiba na hadhi ya kuwakilisha RT ndani na nje ya nchi.
John mwanariadha mahiri wa zamani, aliweka wazi mtiririko wa matukio kuelekea uchaguzi huo, kuwa Novemba 5-11 kuchukua fomu, 12-20 kurejesha fomu, Novemba 21 usaili na kutangaza matokeo jijini Dodoma, Novemba 23-24 kupokea mapingamizi ya wagombea.
Novembaa 24 hadi 27 itakuwa ni kampeni kwa wagombea na tukio lenyewe la uchaguzi.


No comments:
Post a Comment