Waziri Mkuu Kivuli wa Chama cha ACT Wazalendo Doroth Semu akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam.
Na Hussein Ndubikile, Dar es Salaam
CHAMA cha ACT Wazalendo kimetaja mafanikio kiliyoyapata tangu kuundwa kwa Kamati ya Kuisimamia Serikali ya Wasemaji wa Kisekta miezi 10 iliyopita.
Akizungumza na wanahabari jijini Dar es Salaam Waziri Mkuu Kivuli wa ACT Wazalendo Dorothy Semu amesema kwa muda wa miezi 10 wamefanikiwa kutoa matamko rasmi ya kiuchambuzi yapatayo 95 na Mkutano na Waandishi wa habari 31 na ziara za wasemaji wa kisekta (Mawaziri Vivuli) saba.
“Ziara
ya Waziri Mkuu Kivuli kwenye vyombo vya Habari; Ziara ya Mawaziri
Vivuli wa Kilimo, Biashara na Nishati kwenye Mikoa ya Kusini, Ziara ya
Waziri Kivuli wa Madini kutembelea Wachimbaji wadogo Geita; ziara ya
Waziri Kivuli wa Biashara na Viwanda kutembelea ajali ya moto Soko la
Karume; Ziara ya Waziri Kivuli wa Maji na Mazingira kufuatilia maendeleo
ya Mradi wa visima vya maji Kimbiji na Kigamboni; Ziara ya Waziri
Kivuli wa Ardhi, Nyumba na Makazi katika kata ya Bunju na Wazo,” amesema
Semu.
Semu
akibainisha mafanikio hayo amesema kutokana na kupanda kwa gharama za
maisha kutokana na bidhaa mbalimbali kupanda bei walitoa msimamo na
mapendekezo ya kukabiliana na changamoto hizo ili kuleta unafuu kwa
wananchi.
Kwamba
walitoa pendekezo la kupunguza tozo, ushuru na kodi kwa bidhaa
zinazoingizwa kutoka nje ambazo ni muhimu kwa maisha ya watu kama vile
mafuta ya kula, sukari, ngano na mafuta ya petroli na diseli, na
kuongeza uzalishaji wa chakula na mahitaji muhimu kwa nchi huku
wakiitaka Serikali kuongeza umakini wa kudhibiti soko holela la nje
(usafirishaji wa chakula nje) kwa ajili ya kukabiliana na kupanda kwa
bei za bidhaa za chakula.
Licha
ya hapa na pale Serikali ilitekeleza baadhi ya mapendekezo tuliyowahi
kutoa japo sio kwa ufanisi na kwa usahihi kama vile ilitoa ruzuku ya
mafuta na mbolea, kuondoa kodi kwenye mafuta ya kula na kupunguza tozo
za miamala ya kieletroniki (Simu na Benki),” ameeleza Semu.
Hata
hivyo ameeleza kwamba mwenendo wa mfumuko wa bei (gharama za maisha)
bado unazidi kupaa, hivyo, ameitaka Serikali kuweka mikakati ya kuhami
maisha ya watu na kujiandaa kukabiliana na hali hiyo na kuwaandaa
wananchi kuongeza uzalishaji na angalau kukidhi mahitaji ya ndani.
Kuhusu
Miswada ya Sheria na kanuni zilizoenda Bungeni, amesema kupitia Kamati
ya Wasemaji wa kisekta ya kuisimamia Serikali walifuatilia, kuchambua,
kukosoa na kutoa mapendekezo kuhusu miswada kadhaa iliyowasilishwa.
Miongoni
mwa miswada hiyo ni Muswada wa Bima ya Afya kwa wote ambao
uliwasilishwa na Serikali kwa mara ya kwanza bungeni Septemba 2022.
Kwamba
pamoja na nia njema ya Serikali ya kutaka kupanua wigo wa watu walio
kwenye sekta isiyo rasmi kuingizwa kwenye mifumo ya bima, maudhui ya
muswada huo yalikuwa na mapungufu mengi.
“Tatizo
tuliloliona ni kuwa sehemu ya wananchi walio sekta isiyo rasmi
wasingeweza kumudu gharama za bima hiyo kutokana na viwango vya juu
vilivyowekwa. Pia kiuchambuzi na uhalisia muswada ulikuwa unaimarisha na
kukuza madaraja ya kupata huduma bora kama ilivyo sasa, kwa wasio na
uwezo na wenye uwezo,” amesema Semu na kuongeza,
Pia,
mfumo wa uchangiaji kutokuwa na uhakika na endelevu, uliwekeza kwenye
kutumia mabavu kwa kuzuia watu kupata huduma zingine kama njia ya
kuwavutia wananchi kujiunga na Bima ya Afya,”.
Hivyo
amebainisha, ACT Wazalendo kwa kutambua changamoto ya afya, hususani
gharama za matibabu zimekuwa kikwazo kikubwa kwa wananchi wengi.
Kutokana
na umaskini, wengine hawana kipato cha uhakika kinachoweza
kuwahakikishia wanapokuwa na magonjwa kumudu gharama hizo, wachache
(ambao ni watumishi wa Serikali na wengine kwenye Sekta binafsi rasmi)
ndio wenyewe uhakika wa matibabu kupitia Mfuko wa Bima ya Afya ya Taifa
au bima zingine.
Kwamba wananchi wengi wanatumia fedha kutoka mifukoni mwao wanapougua au kupitia Mfuko wa Afya ya Jamii (CHIF).
Amesema,
waliupinga Muswada huo kwa sababu ulikuwa hauendi kuondoa matatizo ya
msingi kwenye upatikanaji wa huduma bora za afya kwa usawa na kwa
uhakika.
“Tuliwaeleza
tatizo la afya ya Watanzania halitokani na kukosa matibabu tu bali ni
mazingira hatarishi ya kazi, watu kukosa vipato vya kueleweka, masikini
kuendelea kuwa maskini zaidi, wazee kutopatiwa mahitaji yao ya msingi,
umaskini wa chakula na kipato,” amebainisha Semu na kusema,
“Mfumo
utakaoimarisha afya ya watanzania na kuwezesha kugharamia matibabu kwa
watu wote nchini ndio jawabu la kuimarisha afya na kukabiliana na
changamoto za gharama za matibau. Sisi tulipendekeza mfumo wa hifadhi ya
jamii kwa watu wote ambao ndani yake ungetoa fao la bima ya afya watu
wote,”.
“Hatimaye Muswada uliondolewa rasmi Bungeni, tunatumai sasa kama wadau tutasikilizana ili kuboresha zaidi,”.
Kuhusu
Kanuni ya Kikotoo cha Mafao ya Uzeeni, amesema Serikali ilirejesha
kanuni hiyo iliyopigiwa kelele mwaka 2019 na kuifanyia marekebisho
madogo.
“Kiukweli,
ACT Wazalendo tulipambana kuhakikisha kanuni hizo zisipitishwe na Bunge
kwa kutoa mapendekezo mbadala kupitia Kamati hii ya wasemaji wa
kisekta,” ameeleza Semu.
Amesema
uamuzi wa Serikali kutangaza Kanuni mpya uliweka kikotoo cha 1/580
badala ya 1540, pia malipo ya mkupuo ya mafao (kiinua mgongo) ya
mtumishi aliyestaafu atalipwa kwa asilimia 33 badala ya 50% iliyokuwa
inatumika kabla, umri wa kuhudumiwa mstaafu ni miaka 12.5 badala ya
miaka 15.5.
Kwamba
walionesha uchambuzi wa athari za kutumia kikotoo kipya chenye
marekebisho madogo tu ya asilimia kutoka 25 hadi 33 na kuacha maeneo
mengine kama yaliyovyo, namna yatakavyoenda kumpunja mstaafu.
“Kutokana
na matatizo ya kanuni za mafao tulizipinga kanuni hizi, kwa kuwa
tunaamini Mfumo wa Hifadhi ya Jamii unapaswa kusaidia kulinda maisha ya
watu na kutoa uhakika wa kuishi vizuri unapokutwa na majanga au kupoteza
uwezo wa kufanya kazi kwa namna yoyote ile,”.
Kuhusu
Muswada wa huduma za Habari amesema waliungana na wanahabari kupaza
sauti kuhakikisha muswada huu unarekebishwa kwamba kazi hiyo wataendelea
nayo mwaka 2023.
No comments:
Post a Comment