December 30, 2022

Askari Polisi Mtwara atwaa bodaboda NMB MastaBata

 

Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Faraja Ng'ingo (kulia) akimkabidhi funguo ya Pikipiki mshindi wa droo ya sita ya NMB MastaBata 'Kote Kote', Charles Shemsanga, kabla ya kuchezesha droo ya saba ya kampeni hiyo inayolenga kuhamasisha matumizi ya kadi badala ya pesa taslimu. Droo hiyo ilifanyika tawi la NMB Bank House jijini Dar es Salaam jana. Kushoto akishuhudia ni Kaimu Meneja wa tawi hilo, Lucas Malua. Katika droo hiyo Husna Juma Baraka wa Mtwara alijishindia Pikipiki, huku washindi 75 wakizawadiwa pesa taslimu Sh. 100,000 kila mmoja. (Na Mpiga Picha Wetu).

Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Faraja Ng'ingo (katikati) akibonyeza kitufe cha kompyuta kuchezesha droo ya saba ya Kampeni ya NMB MastaBata 'Kote Kote', inayolenga kuhamasisha matumizi ya kadi badala ya pesa taslimu. Droo hiyo ilifanyika tawi la NMB Bank House jijini Dar es Salaam jana. Kulia ni Mwakilishi wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Irene Kawili na kushoto ni Kaimu Meneja wa tawi hilo, Lucas Malua. Katika droo hiyo Husna Juma Baraka wa Mtwara alijishindia Pikipiki, huku washindi 75 wakizawadiwa pesa taslimu Sh. 100,000 kila mmoja. (Na Mpiga Picha Wetu).

 

NA MWANDISHI WETU

 

ASKARI wa Jeshi la Polisi mkoani Mtwara, WP Husna Juma Baraka, ameibuka mshindi wa pikipiki katika droo ya saba ya Kampeni ya NMB MastaBata ‘Kote Kote’ inayoendeshwa na Benki ya NMB, ambayo hadi sasa imeshatoa zawadi zenye thamani ya Sh. Milioni 138 kati ya zaidi ya Sh. Mil. 300 zinazoshindaniwa.

 

NMB MastaBata ni kampeni inayohamasisha matumizi ya kadi za NMB Mastercard na Lipa Mkononi (QR Code), badala ya pesa taslimu, ambako droo hiyo ilisimamiwa na Ofisa wa Bodi ya Michezo ya Kubahatisha Tanzania (GBT), Irene Kawili na kufanyika katika Tawi la Bank House.

 

Zawadi zenye thamani ya zaidi ya Sh. Mil. 300 zitatolewa kwa washindi 854 wa kampeni hiyo, wakiwemo 76 wa kila wiki, 51 wa kila mwezi na washindi saba wa ‘grand finale,’ ambako hadi kufikia jana, washindi walionufaika na MastaBata Kote Kote ni 587, wakijinyakulia zawadi zenye thamani ya Sh. Mil. 138.

 

Akizungumza kabla ya droo hiyo, iliyoambatana na makabidhiano ya pikipiki kwa mshindi wa droo ya sita, Charles Shemsanga, Kaimu Meneja wa NMB Kanda ya Dar es Salaam, Faraja Ng’ingo, alisema licha ya kuchagiza matumizi ya kadi, lakini pia wanaitumia MastaBata Kote Kote kurejesha kwa jamii sehemu ya faida yao.

 

“Kupitia kampeni hii, tunawazawadia washindi 75 kila wiki kiasi cha Sh. 100,000 kila mmoja, huku mmoja akitwaa pikipiki, tunatoa pia pikipiki mbili kwa washindi wawili wa kila mwezi – sambamba na washindi 49 wa pesa taslimu Sh. Mil. 1 kila mmoja kwa droo za mwezi.

 

“Katika kuhitimisha kampeni hii, washindi saba (na wenza wao watakaowachagua) watajishindia safari ya Dubai iliyogharamiwa kila kitu na NMB, ambako watakaa kwa siku nne. Hii yote ni katika kuhamasisha matumizi ya kadi, ambayo kimsingi ni salama zaidi, nafuu zaidi kwa wateja wetu,” alisema Faraja.

No comments:

Post a Comment

Pages