December 24, 2022

Ubalozi wa Marekani wawasaidia Wajasiriamali Wanawake wa Bagamoyo

Bagamoyo – Wanawake wajasiriamali kutoka Bagamoyo na Dar es Salaam, leo wamehitimu mafunzo maalumu ya wiki 13 ya biashara na ujasiriamali yaliyofadhiliwa na serikali ya Marekani kupitia programu ya Mafunzo kwa Wajasiriamali Wanawake (Academy of Women Entrepreneurs – AWE). 


Balozi wa Marekani nchini Donald Wright aliwapongeza wanawake hawa na kuwahimiza kutumia ujuzi walioupata kujenga biashara zenye mafanikio. Katika mahafali yaliyohudhuriwa na Mkuu wa Wilaya ya Kisarawe Nickson Simon, aliyemuwakilisha Mkuu wa Mkoa wa Pwani Aboubakar Kunenge, Kaimu Mkuu wa Wilaya ya Bagamoyo, Makamu Mkuu wa Taasisi ya Sanaa na Utamaduni Bagamoyo (TASUBA) Bw. Gabriel Kiiza na wageni wengine waalikwa. 

 AWE ni mpango wa Kimataifa wa Serikali ya Marekani wa kuwawezesha wanawake kiuchumi unaokusudia kuwajengea uwezo wanawake milioni 50 duniani kote kufikia upeo wa uwezo wao kiuchumi. AWE ina dhamira ya dhati ya kuwapa wanawake elimu na ujuzi, kuwajengea mitandao na kufungua fursa wanazohitaji ili kuyabadilisha mawazo yao kuwa miradi halisi ya kujiletea kipato.

 

Akizungumza na wahitimu katika mahafali hayo, Balozi Wright alielezea matokeo ya mafunzo yanayotolewa na AWE. “Mafunzo ya wiki 13 mliyoyapata mkiwa sehemu ya programu hii yamewapa ujuzi kwa vitendo utakaowawezesha kuanzisha biashara endelevu pamoja na kuwaunganisha na wakufunzi (mentors) na wajasiriamali kama ninyi wa nchini Marekani,” alisema.

 

 Aliendelea kusema kuwa kuwajengea wanawake uwezo wa kiuchumi ndio njia ya haraka zaidi ya kuibadilisha jamii. “Jitihada za wanawake huwa na matokeo makubwa zaidi kwa jamii nzima kwa sababu wanawake wanapofanikiwa mara nyingi watawekeza mapato yao katika familia na jamii zao, wakigharamia mahitaji kama vile ada kwa watoto wao na huduma za afya.  Manufaa ya kiuchumi ya mafanikio yenu yanasaidia vizazi vijavyo. Tayari ubunifu wenu unaleta matokeo chanya katika jamii na uchumi wa Tanzania,” alisema.

 

Kundi la wahitimu wa Bagamoyo ni kundi la saba la washiriki wa programu ya AWE.  Kundi la kwanza la wanawake 20 lilihitimu tarehe 9 Septemba, 2019 jijini Dar es Salaam. Kundi la pili lililokuwa na wanawake wajasiriamali 25 kutoka Iringa lilihitimu tarehe 16 Desemba 2020.  

 

Kundi la tatu lililokuwa na washiriki 17 kutoka Zanzibar lilihitimu tarehe 28 Juni 2021. Kundi la nne lililokuwa na washiriki 32 kutoka Mwanza, lilihitimu tarehe 8 Novemba 2021, na kundi la tano lililokuwa na washiriki 31 kutoka Dodoma, lilihitimu tarehe 6 Juni 2022 na kundi la sita lililokuwa na washiriki 32 kutoka Mbeya lilihitimu tarehe 3 Oktoba 2022.

 

Kupitia Ubia na Taasisi ya Marekani ya Maendeleo ya Afrika (U.S. African Development Foundation -USADF), wajasiriamali wanaoshiriki programu ya AWE wanaweza kupatiwa na USADF fedha za mtaji wa hadi Dola za Kimarekani 20,000 ili kupanua biashara zao.


Ubalozi wa Marekani unashirikiana na Selfina kutekeleza programu ya AWE nchini Tanzania. Ikiwa imeanzishwa mwaka 2002 na Dk. Victoria Kisyombe, Selfina ni taasisi ya Kitanzania ya utoaji mikopo midogo midogo iliwalenga zaidi akina mama wajane na wasichana. 

 

Katika miaka 19 iliyopita, Selfina imewawezesha kiuchumi zaidi ya wanawake 31,000 kupitia mikopo inayozunguka. Maisha ya zaidi ya watu 300,000 yameguswa kutokana na faida zilizopatikana kutokana na mikopo hiyo. Wanawake sasa ni wamiliki wa biashara zao wenyewe na zaidi ya nafasi za ajira 150,000 zimetengenezwa.

No comments:

Post a Comment

Pages