December 21, 2022

Wizara ya Maliasili yamtangaza Faru Majaliwa, Balozi Heiss

 NA MAKUBURI ALLY

WIZARA ya Maliasili na Utalii imewatangaza Faru wawili majina ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa na Balozi wa Ujerumani hapa nchini Regine Heiss walioko kwenye mbuga za wanyama hapa nchini.



Hatua hiyo imefikiwa kwenye hafla ya makabidhiano ya magari 51 aina ya Land Cruiser yenye thamani ya Shilingi Bilioni 15 yaliyokabidhiwa kwa Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa kwa Wizara ya Maliasili na Utalii chini ya mradi wa msaada wa dharura kwa uhifadhi na utalii Tanzania, hafla iliyofanyika kwenye ukumbi wa mikutano wa Julius Nyerere jijini Dar es Salaam.


Waziri wa Maliasili na Utalii Balozi, Pindi Chana alisema Faru Majaliwa alizaliwa Januari mwaka huu huku Faru Hess alizaliwa Februari mwaka huu ambao ni zao la Faru Rajabu.


Balozi Pindi Chana baada ya kufanikisha hatua hiyo ya kuwapa majina ya Waziri Mkuu na Balozi wa Ujerumani, wadau wengi wameonesha kuhitaji na wao majina yao yatumike kwa wanyama wengine ambako alitoa wito kwa kila mwenye kuhitaji afika Mamlaka ya Hifadhi za Taifa (TANAPA) ili waweze kuchangia hatua hiyo.


Hatua ya makabidhiano hayo kwa waziri Mkuu magari hayo ambayo pia aliyakabidhi kwa Wizara ya Maliasili na Utalii ni msaada wa dharula kwa uhifadhi na utalii katika mbuga za Serengeti, Nyerere pamoja na Selous ambapo yatatumika kwa ajili ya kufanyia doria kuleta ujirani mwema pamoja na kuimarisha mawasiliano ndani ya mbuga hizo.


Akizungumza kwenye katika hafla ya makabidhiano, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, alisema Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan, amefurahishwa na jitihada za Wizara ya Maliasili na utalii na ameipokea kwa furaha taarifa hii ya msaada kutoka nchini Ujerumani.
“Rais Samia ana matumaini mahusiano ya Ujerumani na Tanzania yataendelea na  anaamini Wizara ya Maliasili na utalii na bodi zake zinafanya vizuri jitihada zenu zitakuwa endelevu na kuifanya iwe ya ushindani zaidi,” 


“Nataka nimtoe wasi wasi Balozi Regine Heiss kuwa awe na amani magari hayo yatatumika kwenye Wizara ya Maliasili na utalii pekee wala hayatapelekwa kwenye wizara nyingine,” alisema Majaliwa.
Alisema pia Serikali ya Tanzania ipo kwenye mchakato wa kununua ndege moja na Helkopta kwa ajili ya kupambana na majanga mbalimbali lakini pia wataendelea kushirikiana na jumuiya za kimataifa kukabiliana na changamoto mbalimbali za mabadiriko ya tabia nchi.


“Ushirikiano wa Tanzania na Ujerumani ni wa kihistoria ambao uliasisiwa na baba wa taifa mwalimu Julius Kambarage Nyerere ambao umekuwa ukibadirika kulingana na nyakati ,” alisema Majaliwa.
Naye Balozi wa Ujerumani nchini Tanzania Regine Heiss, alisema kuwa anafuraha kukabidhi magari hayo kwa serikali ya Tanzania kwaajili ya kusaidia kukabiliana na changamoto mbalimbali kwenye sekta ya utalii.


“Novemba mwaka jana Ujerumani ilikaa na kuangalia ni jinsi ya kuisaidia Tanzania kwenye sekta ya utalii kwa kukabiliana na ujangili  mabadiriko ya tabia nchi pamoja na kuangalia matumizi bora ya ardhi kwa kuondoa mimea vamizi,”


Alisema kuwa amefurahi kuona serikali ya Ujerumani na Tanzania zimeunganisha nguvu pamoja kupambana majanga mbalimbali yanaoikumba sekta ya utalii.

No comments:

Post a Comment

Pages