Waziri wa Madini, Dkt. Doto Biteko amewasisitiza wachimbaji wa madini nchini kuzingatia Sheria, Kanuni, Taratibu na Miongozo inayosimamia Sekta ya Madini ili wachimbe rasilimali hiyo kwa manufaa ya wachimbaji na jamii kwa ujumla.
Dkt. Biteko
amesema hayo Januari 3, 2023 katika ziara yake Wilayani Nyang'hwale mkoa
wa Geita alipotembelea na kuzungumza na wachimbaji wadogo katika mgodi
wa dhahabu wa Isonda.
Amewataka
wachimbaji kuheshimu maeneo yenye leseni ili kuepusha migogoro
inayojitokeza mara kwa mara kwa wawekezaji wa madini katika maeneo
yenye shughuli za uchimbaji.
"Mwenye leseni anawajibu wa kulinda leseni yake na sisi tuna wajibu wa kutovamia leseni ya mtu mwingine," amesema Dkt. Biteko.
Vilevile,
amewataka wachimbaji katika mgodi wa Isonda wanaochimba katika leseni
hiyo ya utafiti kutomsumbua mwekezaji huyo kutoka kampuni ya Henan
Yukuang International Mining Investment Ltd ili wasitolewe katika eneo
hilo.
Aidha, amemuagiza
Mkuu wa Wilaya hiyo na Afisa Madini kusimamia shughuli hizo ili
wachimbaji wachimbe kwa amani na kampuni ya Henan ifanye utafiti.
Akieleza
namna Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan anavyowapenda wachimbaji, amesema
kuwa Rais amemuelekeza mara nyingi kuwalea wachimbaji wadogo ili
wachimbaji hao wafanikiwe.
Amesema,
Serikali itaendelea kutoa maeneo mengine kwa wachimbaji nchini ili
kuendelea kuchimba rasilimali hiyo iliyopo nchini na kubadilisha maisha
yao.
Aidha, ameutaka
uongozi wa mgodi huo kukutana na Serikali ya kijiji ili mgodi huo uandae
mpango wa kuchangia huduma za jamii ili wananchi wanaozunguka eneo la
mgodi huo wanufaike.
Akizungumza
suala la ukwale, Waziri Biteko ameagiza wanawake wanaojihusisha na
ukwale kuacha kusumbuliwa ili wafanye shughuli zao vizuri na
kuhahakikisha wale wote wanaojihusisha na wizi wanaacha mara moja.
Ukwale ni mawe ya madini yanayosadikika kuwa na kiasi kidogo sana cha madini ya dhahabu.
Aidha, amemuagiza Afisa Madini Mkazi wa Mbogwe kusimamia suala hilo ili shughuli ya ukwale ifanyike bila usumbufu.
Naye,
Mwakilishi wa Mkuu wa Wilaya ya Nyang'hwale, Fabian Sospeter amesema
kuwa, shughuli za uchimbaji madini zinazofanyika katika wilaya hiyo
zimesaidia kuongeza mapato ya Halmashauri ambapo hadi sasa kiasi cha
Shilingi bilioni 1.5 kati ya malengo ya bilioni 1.9 zimekusanywa na kati
ya hizo, Shilingi bilioni 1 imetokana na shughuli za madini.
Ziara
hiyo ya kutembelea mgodi wa Isonda na eneo lenye mgogoro wa mpaka
kijiji cha Kharumwa na Izunya imehudhuriwa na Wataalamu kutoka Wizara ya
Madini, Tume ya Madini, Afisa Madini Mkazi Mbogwe na wataalam wa
Halmashauri ya Wilaya ya Nyang'hwale.
No comments:
Post a Comment