January 09, 2023

KMC FC KUWAKOSA WACHEZAJI SABA, IKIJIWINDA NA MTIBWA SUGAR



Na Mwandishi Wetu


Wachezaji wa Timu ya KMC FC wamereja kambini na leo kuanza maandalizi kuelekea katika mchezo unaokuja wa Ligi Kuu ya NBC soka Tanzania Bara dhidi ya Mtibwa Sugar utakaochezwa Januari 13 katika uwanja wa Manungu Mkoani Morogoro.



Timu hiyo ya Manispaa ya Kinondoni imeingia kambini jana ikijiandaa na Mtibwa Sugar ambapo itakuwa ugenini na kwamba Kocha Mkuu Thierry Hitimana ambaye pia alikuwa Rwanda kutokana na kufiwa na Mdogo wake pia ameingia na kuanza kukinoa kikosi hicho leo.


Aidha katika kikosi hicho cha wana Kino Boys wachezaji wote wamerejea huku ikiwakosa wachezaji saba kutokana na sababu mbalimbali ambao ni  Sadalah Lipangile, Ibrahimu Ame, Matheo Anton, Steve Nzingamasabo pamoja na  Ismail Gambo ambapo wote ni kutokana na changamoto za kifamilia huku Emmanuel Mvuyekure na Hance Masoud wakiendelea kupatiwa matibabu kutokana na  majeraha yamuda mrefu.


" Tumeanza mazoezi leo baada ya mapumziko mafupi ambayo tuliwapa wachezaji katika kipindi hiki ambacho Timu zipo kwenye mapumziko kupisha michuano ya Kombe la Mapinduzi, kikubwa tunakwenda kwenye mchezo mgumu ambao tutakuwa ugenini na ndio mana tumekuwa na muda mfupi wakupumzika lengo likiwa kujiandae vizuri kwa ajili ya kupata matokeo chanya.


Tutakuwa na mchezo mgumu ambapo ukizingatia tutakwenda tena ugenini baada ya kutoka kupoteza dhidi ya Ihefu Januari tatu mwaka huu, lakini tunafurahi kuwa wachezaji wetu wamerudi kwenye viwango vizuri hata kwenye mazoezi wanafanya wakiwa na hari na morali nzuri ambayo inaleta taswira njema kuelekea kwenye mchezo wetu dhidi ya Mtibwa Sugar.


KMC FC inakwenda kwenye mchezo wa mzunguko wa 20 ikiwa kwenye nafasi ya tisa mwa msimamo wa Ligi Kuu ya NBC ikiwa na jumla ya alama 22 na kwamba mashabiki na Watanzania wote ambao sikuzote wamekuwa wakiisapoti pindi inapokuwa uwanjani tutakwenda kupambana katika michezo iliyobaki na kufanya vizuri.

No comments:

Post a Comment

Pages