January 15, 2023

RT LAWAMANI KUKACHA CROSS COUNTRY ARUSHA

 


RAIS WA RT, SILAS ISANGI.

Matukio mbalimbali fainali ya mbio za Nyika Mkoa wa Arusha, January 14 viwanjs vya Ilboru.



NA MWANDISHI WETU, ARUSHA


MKOA wa Arusha umekamilisha mtiririko wa mashindano yake ya Mbio za Nyika kwa mafanikio Januari 14 kwenye viwanja vya Ilboru huku Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), likitupiwa lawama kwa kutoonesha ushirikiano kwa mkoa wake mwanachama.

 

Chama cha Riadha Mkoa wa Arusha (ARAA), kimeendesha mtiririko wa mashindano hayo kwa nyakati tofauti na Januari 14, ndio ilikuwa fainali kwa mbio za Kilomita 10 Wanaume na Wanawake, ambako mgeni Rasmi alikuwa Meya wa Jiji la Arusha, Mh. Maxmillian Iranqhe, huku ikishuhudiwa wanariadha mbalimbali ikiwemo maarufu wakichuana vikali.

 

Wakati Mataifa yote duniani yakijipanga kuelekea Mashindano ya Dunia ya Mbio za Nyika, yanayotarajiwa kufanyika nchini Australia hivi karibuni, Tanzania maandalizi yake yamepoa, ambako ni Mkoa wa Arusha pekee, ambao umeonyesha uhai, jambo ambalo lilitegemewa na wadau wengi wa mchezo wa Riadha lingeungwa mkono na RT, lakini imekuwa kinyume, kwani licha ya kutotoa sapoti yoyote, pia hakukuwa na mwakilishi yoyote kutoka shirikisho aliyehudhuria tukio hilo, jambo ambalo wadau wamebaki na viulizo na kuhoji utendaji wa viongozi waliopewa dhamana ya uongozi.

 

Mbio hizo zilipewa sapoti na Baraza la Michezo la Taifa (BMT), Wanariadha maarufu Alphonce Simbu, Gabriel Gray, wadau Rais mstaafu Francis John, Mwanariadha mahiri wa zamani na Kocha wa mchezo huo, Moris Okinda, Mwenyekiti mstaafu Kamisheni ya Wanariadha Amani Ngoka na wengineo, huku RT ikiwa imeingia mitini.

 

"Tunapenda kuwapongeza Arusha kwa kuwa mfano katika mchezo wa Riadha Tanzania, bila kupepesa RT ichukue mashindano haya kama ya Taifa, na mikoa mingine iige mfano wa Arusha, lakini tunasikitika kwa kutoliona shirikisho mchango wake licha ya mlezi wa vyama BMT kuwepo...," alinukuliwa Mwanariadha wa zamani na Kocha Suleiman Nyambui, kauli ambayo imeendana na wadau mbalimbali wakitoa lawama zao kwa RT chini ya Rais wake Silas Isangi, kutokana na kitendo hicho walichokitafsiri kama shirikisho hilo kutokuwa na nia ya dhati ya kuendeleza mchezo huo nchini Tanzania.

 

Juhudi za kuwatafuta viongozi wa RT, ambapo hata mjumbe wake mahsusi anayewakilisha Kanda ya Kaskazini, akiwa pia mkazi wa Arusha, Alfredo Shahanga, ziligonga ukuta na bado zinaendelea kuelezea sintofahamu hii.

 

Kaimu Katibu Mkuu wa RT, Wakili Jackson Ndaweka, yuko nchini Ethiopia akihudhuria Mkutano wa Kanda ya Afrika Mashariki na Kati (EAAR), huku Rais Isangi ambaye makazi yake yapo jijini Mwanza, alipotafutwa kwa simu hakupatikana na hata alipotumiwa ujumbe mfupi, hakujibu hadi Habari Mseto inapokwenda mitamboni.

 

Katika mbio hizo, Inyasi Sulle aliibuka mshindi kwa wanaume akitumia dakika 33:12.44 akifuatiwa na Fabian Nelson wa Jeshi la Polisi 33:45.52 na Mathayo Sombi wa Arusha 33:52.85.

 

Kwa wanawake, Magdalena Shauri wa JWTZ alishinda akitumia 39:58.20 akifuatiwa na Maycelina Mbua 42:01.95 huku nafasi ya tatu ikienda kwa Valentina Michael 43:36.58 wote kutoka JWTZ. 

No comments:

Post a Comment

Pages