January 04, 2023

    SEKTA YA BARABARA RUVUMA YATENGEWA SHILINGI BILIONI 46.35


SERIKALI ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan imetenga shilingi bilioni 46.35 kwa ajili ya sekta ya barabara mkoani Ruvuma.

 


Mkuu wa Mkoa wa Ruvuma Kanali Laban Thomas amesema fedha hizo zimetengwa katika bajeti ya  mwaka 2022/2023 na kwamba kati ya fedha hizo zilizopokelewa hadi sasa ni  shilingi bilioni 14.02 sawa na asilimia 30.43.

Hata hivyo amesema  Wakala wa Barabara TANROADS katika bajeti hiyo wametengewa shilingi bilioni 22.588 ambapo hadi sasa wamepokea shilingi bilioni 7.17 na  Wakala wa Barabara Vijijini na mijini (TARURA) wametengewa shilingi bilioni 23.76 na wamepokea shilingi bilioni 6.85 sawa na asilimia 29.

“Tangu serikali ya Awamu ya Sita iingie madarakani tumeshuhudia namna ambavyo Mkoa wetu wa Ruvuma unavyonufaika katika sekta ya barabara,kwa sababu serikali imekuwa inatenga fedha za kutosha katika sekta ya barabara’’,alisisitiza RC Thomas.

Mkuu wa Mkoa amemshukuru Rais Dkt.Samia Suluhu Hassan kwa kuwezesha mpango wa utekelezaji wa maendeleo ya barabara ambapo  wilaya zote za Mkoa wa Ruvuma zimeunganishwa kwa barabara za lami na hivi sasa uunganishaji wa barabara za lami ndani ya wilaya unaendelea.

Kwa upande wake Meneja wa TANROADS Mkoa wa Ruvuma Mhandisi Ephatar Mlavi amesema serikali inatarajia kuanza Ujenzi wa Barabara ya Songea – Makambako kwa kiwango cha lami na sehemu ya Songea–Lutukira ikujumuisha na sehemu ya Mtwara korido yenye urefu wa kilometa 111.

 

Amesema  Serikali tayari imeshaingia makubaliano na Mfadhili Benki ya Dunia na hivi sasa hatua mradi upo katika hatua za awali za manunuzi.

 

“Mradi huu utahusisha ujenzi wa kilometa 111 za lami ambazo zitajumuisha kilometa 14 za Songea bypass (Mtwara Corridor) na Songea–Lutukira kilometa 97’’,alisema Mhandisi Mlavi.

 

Kwa upande wake Meneja wa Mkoa wa Barabara za vijijini na mijini (TARURA) Mhandisi Wahabu Nyamzungu ameutaja mtandao wa barabara Mkoa wa Ruvuma una mtandao wa barabara zenye urefu wa kilometa7,146.22 ukijumuisha barabara za lami,changarawe na udongo.

Hata hivyo amesema serikali kupitia TARURA inaendelea kufanya jitihada za kuhakikisha mtandao wote wa barabara katika Mkoa mzima unapitika katika misimu yote ya mwaka.

 


No comments:

Post a Comment

Pages