January 12, 2023

 Shughuli za kibinadamu ikiwemo kilimo zatajwa chanzo kuathiri shoroba mbalimbali nchini

Waandishi wa habari za mazingira wakiwa katika picha ya pamoja. Wanahabari hao wapo wilayani Bagamoyo kwa mafunzo ya Mradi wa 'Tuhifadhi Maliasili' unaoratibiwa na Chama cha Waandishi wa Habari za Mazingira Tanzania (JET) chini ya ufadhili wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID).



NA JANETH JOVIN

SHUGHULI za kibinadamu ikiwemo kilimo zimebainika kuwa ni moja ya vitu vinavyoathiri maeneo yanayounganisha hifadhi mbalimbali nchini (shoroba) ambazo zinatumika kupita wanyamapori lakini pia kwa matumizi mengine ya binadamu.


Hayo yamebainishwa leo wilayani  Bagamoyo mkoani Pwani na Dk. Elikana Kalumanga ambaye ni Meneja Ushirikishwaji wa Sekta Binafsi wa Mradi wa Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID) wa Tuhifadhi Maliasili, wakati wa mafunzo kwa waandishi wa habari za mazingira kuhusiana na mradi huo.


Dk.Kalumanga alisema shoroba hizo zimekuwa zikiathiriwa na shughuli hizo za binadamu na kuhatarisha uwepo wa maeneo hayo na maisha ya wanyama hao kwa ujumla.


"Kwa sasa hali za shoroba zetu mbalimbali nchini si nzuri kwani kwa mujibu wa takwimu za serikali zipo baadhi zimepotea kabisa kutokana na shughuli hizo za wananchi zinazofanywa kila siku, kuna haja ya kuendelea kuwaelimisha wananchi, " alisema


Hata hivyo alisema kupitia mafunzo hayo yaliyoratibiwa na Chama cha Waandishi wa Habari wa Mazingira Tanzania (JET) chini ya ufadhili wa USAID, amewataka waandishi wa habari kuwa mstari wa mbele kuibua na kuelimisha jamii juu ya athari zitokanazo na shughuli hizo za kibinadamu ndani ya shoroba pamoja na faida za kiuchumi zinazopatikana.


"Kwenye shoroba hizi wananchi wanapata vitu vingi kama kuni na dawa, mfano shoroba ya Laja inayotoka hifadhi ya Taifa ya Manyara kuelekea eneo la hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro, kule utawakuta hawa ndugu zetu wa Wahadzabe ambao wanatengemea maeneo hayo kupata rasilimali zao za kila siku ikiwemo chakula na makazi.


"Katika shoroba hizi uwepo tu wa wanyamapori wanawavutia watalii hivyo upo uwekezaji wa hoteli mbalimbali ambazo zinatoa ajira kwa watanzania na wapo wananchi wameweka bidhaa zao za asili na kuwauzia wazungu na watalii wengine, " alisema Dk. Kalumanga


Kwa upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa JET,  John Chikomo alisema kumekuwa na ongezeko la Tembo jambo ambalo limechangiwa kwa kiasi kikubwa na uhifadhi wa wanyamapori.


"Hata ongezeko la watalii wanaoingia nchini ni mafanikio yanayotokana na elimu ya uhifadhi wa mazingira na wanyamapori inayotolewa mara kwa mara kwa waandishi wa habari hapa nchini," alisema.

No comments:

Post a Comment

Pages