January 28, 2023

TAASISI YA JAKAYA MRISHO KIKWETE FOUNDATION KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUBORESHA UTOAJI WA ELIMU NCHINI


Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Angellah Kairuki akizungumza na Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi Jakaya Mrisho Kikwete Foundation (JKMF) Rais Msaafu Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete katika Kikao kilicholenga kuboresha utoaji wa elimu nchini, Leo tarehe 27 Januari 2023 jijini Dodoma. 

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa, Mhe. Angellah Kairuki akiwa katika picha ya pamoja na  Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi Jakaya Mrisho Kikwete Foundation (JKMF) Rais Mstaafu, Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete pamoja na  Kaimu Mkurugenzi wa ElimuMsingi Ofisi ya Rais TAMISEMI, Bi. Suzan Nusu (kushoto), Afisa Mtendaji Mkuu wa Taasisi Jakaya Mrisho Kikwete Foundation, Vanessa Anyoti (wa tatu kulia), Mtakwimu Mkuu wa Serikali, Bi Albina Chuwa (wa pili kulia). Leo tarehe 27 Januari 2023 jijini Dodoma. 



Na Eliud Rwechungura - OR TAMISEMI


Ofisi ya Rais - TAMISEMI inatarajia kuanzisha ushirikiano na Taasisi Jakaya Mrisho Kikwete Foundation (JKMF) unaolenga kuanzisha mpango maalum wa kutoa ajira ya muda mfupi kwa walimu wa kujitolea watakaofundisha Shule za  msingi za Serikali kwa kipindi kisichopungua miaka miwili.


Lengo hilo la ushirikiano limejadiliwa leo katika kikao cha pamoja kati ya Mwenyekiti wa Bodi ya Taasisi ya JMKF, Rais Mstaafu Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete na Mhe. Angellah J. Kairuki (Mb), Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais TAMISEMI kilichofanyika Dodoma leo tarehe 27 Januari 2023.


Katika kikao hicho, pamoja na mambo mengine , Mhe. Dkt. Kikwete ameishauri Ofisi ya Rais TAMISEMI katengeneza kanzidata ya Walimu wote wanaojitolea nchini na kuandaa muongozo wa utakaosimamia mchakato wa kuwapata walimu wa kujitolea na kuratibu maslahi yao. 


Mhe. Dkt. Kikwete ameelezea utayari wa Taasisi ya JMKF kushirikiana kwa karibu na Serikali kutekeleza mpango huo ambao tayari Taasisi hiyo imejipanga kuanza kuutekeleza kwa kushirikiana na Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF) na wadau wengine.


Kupitia kikao hicho, Mhe Dkt Kikwete aliomba Serikali iweke utaratibu mzuri wa kuwaajiri walimu wa kujitolea watakaomaliza muda wao wa kujitolea ili kufanya mpango huo uwe endelevu.


Waziri Mhe. Angellah Kairuki alimweleza pia Mhe. Dkt. Kikwete kuwa Ofisi ya Rais TAMISEMI imejipanga kuboresha sekta ya elimu kwa kuanzisha utoaji elimu kidijitali kwa kuanzisha maabara za TEHAMA katika shule zote za Serikali hapa nchini, ambapo kwa kuanzia shule mpya zote zinazojengwa zitaunganishwa na mfumo wa intaneti ili kufikia lengo hilo. 



Aidha, Waziri Angellah Kairuki alipongeza Taasisi ya JMKF kwa kuanzisha programu ya kutoa elimu kidijitali na kuwa tayari kushirikiana na Serikali katika eneo hilo.


Waziri Kairuki alihitimisha kwa kuishukuru Taasisi ya JMKF kwa jitihada zake za kuiunga mkono Serikali ya Awamu ya Sita katika kuendeleza na kuboresha sekta ya elimu nchini na ameahidi  kuwa Ofisi ya Rais TAMISEMI itaendelea kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Taasisi hiyo na wadau wengine wa sekta binafsi na washirika wa maendeleo wanaoiunga mkono Serikali katika kuimarisha sekta ya elimu.

No comments:

Post a Comment

Pages