March 21, 2023

CCM ZANZIBAR YAWATAKA WAFANYABIASHARA KUFUATA BEI ELEKEZI WAKATI WA RAMADHANI

 NA IS-HAKA OMAR, ZANZIBAR

 

KATIBU wa Kamati Maalum ya NEC, Idara ya Itikadi na Uenezi CCM Zanzibar Khamis Mbeto Khamis, amewashauri wafanyabishara nchini kutopandisha bei za bidhaa za vyakula katika mfungo wa mwezi wa Ramadhani unaotarajiwa kuanza hivi karibuni.

Ushauri huo ameutoa katika mwendelezo wa ziara yake kwenye vyombo vya Habari visiwani Zanzibar,amesema kuna baadhi ya wafanyabishara wamekuwa wakitumia vibaya fursa ya mwezi wa Ramadhani kwa kujinufaisha wenyewe badala ya kuzingatia kipato cha wananchi.

Mbeto, aliitaka serikali kuchukua hatua za kufanya mazungumzo na wafanyabishara hao ili wasikiuke utaratibu wa kufuata bei halali na elekezi iliyowekwa na serikali katika uuzaji wa biashara zinazotokana na mazao ya Vyakula.

Katika maelezo yake Katibu huyo wa NEC Mbeto,alisema waumini wa dini ya kiislamu nchini wanatarajia kuingia katika mfungo huo hivyo taasisi zinazohusika na masuala ya vyakula na miundombinu ya maji watatue changamoto za sekta hizo mapema.

Akizungumzia utekelezaji wa Ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025,alisema Chama kimejipanga vyema  kuisimamia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar katika kutekeleza ilani ya uchaguzi.

Alisema serikali imetekeleza ilani ya uchaguzi Kwa kujenga hospitali 11 za kisasa na zenye vifaa vyote.

Mbali na hilo, alisema serikali tayari imekwishatoa ajira ya watumishi wa sekta ya afya 250 kama ilivyoelekeza kwenye ilani ya uchaguzi.

Alisema asilimia 13.8  ya bajeti Kuu ya  serikali imepelekwa kwenye miradi ya maendeleo jambo ambalo halijawakutokea.

Pia, alisema katika sekta ya elimu serikali ya awamu ya nane imeshajenga shule tisa za ghorofa za msingi katika maeneo ya Unguja na Pemba.

"Serikali ya Mapinduzi ya awamu ya nane pia imeshatoa sh.bilioni 16.5 kwa wajasiriamali katika kuwawezesha kufanya shughuli zao za kila siku, "alisema

Katika maelezo yake Katibu huyo alisema ni kweli kuwa upatikanaji wa huduma za maji katika maeneo mengi visiwani hapa ni changamoto.

Alisema licha ya kuwepo kwa changamoto hizo serikali imeshaanza kutafutia ufumbuzi suala hilo mbapo tayari imeshatoa sh.bilioni 34.5 kwa ajili ya kujenga miundombinu ya maji.

Mbali na hilo, Katibu huyo alihiakikishia Idara ya Habari Maelezo kuwa taarifa za matukio makubwa yanayofanywa na CCM yatafikishwa katika Idara hiyo Kwa ajili ya kutoa taarifa kwa vyombo vya habari.

Aliwapongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt.Samia Suluhu Hassan pamoja na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk.Hussein Mwinyi, kwa kazi kubwa waliofanya ya kutekeleza kwa ufanisi na vitendo ilani ya CCM ya mwaka 2020/2025, ambayo ni mkataba wa miaka mitano baina ya Wananchi na Chama.

Naye Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo Zanzibar Hassan Khatib Hassan alisema kuna eneo la maofisa habari bado halijatumika vizuri.

"Changamoto ambazo wanakutanazo maofisa hawa ni ufinyu wa bajeti kwa kukosa vifaa vya kufanyia kazi,"alisema 

Mkurugenzi huyo alisema endapo maofisa hao wakifanyiwa hivyo watasaidia katika kutoa taarifa za serikali kwa ufasaha.

"Tunaomba suala hili ulichukue na kulipeleka sehemu husika kwani hawa maofisa habari watasaidia kutoa taarifa za viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri kwa kuelezea kazi za Rais," alisema.

Pia, Mkurugenzi huyo alisema Idara ya Habari imefarijika kuona CCM   inavyothamini mchango wa vyombo vya habari visiwani hapa katika kutoa taarifa kwa wananchi.

Naye Naibu Mkurugenzi wa Zenjbar TV (Online) Aboubakar Harith, alisema kituo hicho kimekuwa mstari wa mbele katika kutangaza matukio mbalimbali ya shughuli za Serikali na Chama kwa ujumla.

No comments:

Post a Comment

Pages