March 18, 2023

MNYAMA AMRARUA HOROYA KWA MKAPA 7-0

Na John Richard Marwa

Wamelowa, wamelowa, walowa na mvua, ndivyo unaweza kuelezea mara baada ya AC Horoya kukutana na kipigo kizito kutoka kwa Mnyama Simba wa Msimbazi.



Ni historia imeandikwa kwa Simba kushinda mabao mengi zaidi katika michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika CAFCL hatua ya makundi kwa kipigo hicho kizito walichokitoa kwa AC Horoya katika Dimba la Benjamin Mkapa mchezo wa kundi C.

Ushindi huo umeifanya Simba kutinga Robo Fainali msimu huu wakifikisha pointi 9 nafasi ya pili nyuma ya vinara Raja Casablanca ya Morocco.

Mwalimu Robert Oliveira aliingia kwenye mchezo huo na mpango mkakati ambao umeiwezesha Simba kuutawala mchezo kwa dakika 90 za mchezo licha ya ubora wa kikosi cha AC Horoya na upinzani walioutoa katika mechi ya leo.

Clatous Chota Chama Mwamba wa Lusaka hakika huyu ni Mwamba haswa ameweka kambani mabao matatu 'hat trick ' sambamba na kiwango bora alichokionyesha.

Chama ambaye katika michezo ya raundi ya nne alitwaa tuzo ya mchezaji bora wa Afrika katika mzunguko huo, leo anaibeba Simba mavegani kwa misimu mitatu tofauti Chama anaipeleka Simba Robo Fainali ya michuano ya CAF.

Mabao mengine ya Simba yamewekwa kimiani na mshambuliaji Jean Baleke ambaye ameingia kambani mara mbili huku Sadio Kanoute naye akiweka misumali miwili katika ushidi huo mnono dhidi ya Horoya AC jioni ya leo.

Horoya sio kama walikuwa wabovu ila waliingia kwenye mfumo wa Simba na kuondoka na kapu hilo la mabao.

Katika kundi C mchezo mwingine Vipers ya Uganda wametoka sare ya bao moja kwa moja dhidi ya Raja Casablanca ya Morocco. Matokeo hayo yanaifanya Raja kusalia kileleni na pointi zao 13, Simba nafasi ya pili poini 9, AC Horoya nafasi ya tatu alama 4 huku Vipers wakibuluza mkia na pointi zao mbili kila timu ikisaliwa na mchezo mmoja.


No comments:

Post a Comment

Pages