Naibu Waziri wa Ujenzi na Uchukuzi, Atupele Mwakibete.
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAZIRI wa Ujenzi na Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa amesema uchumi wa nchi unategemea zaidi sekta zinazoathiriwa na hali ya hewa.
Akizungumza jijini Dodoma leo Machi 23,2023 kwa niaba ya Waziri Profesa Mbarawa, Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakabete alisema kwa kuzingatia hilo, utoaji wa huduma bora za hali ya hewa umekuwa kipaumbele cha serikali katika awamu zote.
Alisema hatua hizo zina umuhimu mkubwa na kuongeza tija katika maendeleo ya sekta zote za kijamii na kiuchumi ikiwemo kilimo, utalii, miundombinu, uvumi, mifugo na nishati.
Naibu Waziri Mwakibete alisema hayo wakati wa maadhimisho ya siku ya Hali ya Hewa Duniani (WMD), ambapo Tanzania na nchi nyingine 193 duniani zimeungana kuadhimisha siku hii iliyoasisiwa na Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO).
Maadhimisho ya siku ya hali ya hewa duniani yameadhimishwa yakibeba kaulimbiu isemayo ‘Mustakabali wa Hali ya Hewa, Tabianchi na Maji kwa Vizazi Vyote’.
“Maadhimisho hayo yanaangazia pia mustakabali wa huduma hizi kwa vizazi vyote, upimaji na ubadilishanaji wa data na utaalamu kwa lengo la kukuza ushiriki wa wanasayansi, watoa maamuzi na vijana katika uzalishaji na matumizi ya taarifa sahihi za hali ya hewa na rasilimali maji.
“Utoaji wa huduma za hali ya hewa hapa nchini ulianza kabla ya uhuru, upimaji wa hali ya hewa ulianza mwishoni mwa miaka ya 1800... mfano kituo cha kwanza cha hali ya hewa hapa nchini, kilianzishwa mwaka 1892 katika mji wa Bagamoyo.
“...Jumuiya ya Hali ya Hewa Duniani inatumia siku hii kuadhimisha siku ambayo mkataba wa kuanzishwa kwa Shirika la Hali ya Hewa Duniani (WMO) ulisainiwa, Machi 23,1950 ikiwa ni miaka 73 tangu kuanzishwa kwa WMO.
“Kuadhimisha Siku ya Hali ya Hewa Duniani, tunaadhimisha miaka 150 ya Shirika la kwanza la Kimataifa la Hali ya Hewa (International Meteorological Organization-IMO) ambalo ni mtangulizi wa WMO lililoanzishwa mwaka 1873,” alisema Naibu Waziri Mwakibete.
Kwa mujibu wa Mwakibete, athari za mabadiliko ya hali ya hewa zimeendelea kutatiza uzalishaji na maendeleo katika sekta zinazotegemea zaidi hali ya hewa kijamii na kiuchumi hali inayosababisha sekta hizi kutokuwa na maendeleo endelevu na ya uhakika.
Ili kukabiliana na changamoto hizo, naibu waziri huyo alisema zinahitajika jitihada na hatua za makusudi na endelevu ikiwemo kujenga taasisi madhubuti kwa ajili ya kuboresha na kutoa huduma bora za hali ya hewa hapa nchini.
“Nawapongeza kwa dhati Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA), kwa kutekeleza vema majukumu yenu na kuwa sehemu ya kuaminika ya kupata taarifa sahihi za hali ya hewa.
Alisema serikali itaendelea kushughulikia mapungufu na mahitaji yanayohusu utoaji wa Huduma za Hali ya Hewa nchini kwa nia ya kuboresha huduma za tahadhari zinazoendana na kasi na kukabiliana na maendeleo ya kimataifa ya sayansi na teknolojia, pia katika kuunga mkono mpango wa Umoja wa Mataifa wa kuhakikisha kuwa tahadhari za hali ya hewa zinawafikia watu wote duniani kote.
Alisisitiza kwamba mpango huu unalenga kuhakikisha kwamba kila mtu alindwe kwa kupata taarifa za tahadhari ndani ya miaka mitano kuanzia mwaka 2022.
No comments:
Post a Comment