March 16, 2023

RC KAGERA AWATOA HOFU WANANCHI JUU YA UVUMI UNAOSAMBAA MITANDAONI


Mkuu wa Mkoa  wa Kagera Albert Chalamila akizungumzia Taharuki hiyo mbele ya waandishi wa habari.

 

Na Lydia Lugakila, Bukoba

Mkuu wa Mkoa wa Kagera Albert Chalamila amewatoa hofu wananchi mkoani humo juu ya taarifa yenye Taharuki inayoonekana kusambaa katika mitandao ya kijamii tangu asubuhi yenye ujumbe ulioandikwa na watu mbalimbali  ukieleza kuwa kuna watu wa familia moja wamefariki dunia kwa kile kinachodaiwa kuwa ni ugonjwa wa Ebola.

Chalamila ametoa kauli hiyo Machi 16, 2023 majira ya saa moja usiku wakati akiongea na Waandishi Habari Ofisi kwake.

Chalamila amesema kuwa baada ya Serikali ya Mkoa kwa Kushirikiana na wataalam wa Afya kupata ujumbe huo kutoka mitandaoni wamefanya hatua za haraka za kufika katika maeneo yanayotajwa ili kufanya uchunguzi wa kina na kubaini kinachochunguzwa kama ni kweli.

"Mimi mkuu wa Mkoa baada ya taarifa hizo nimefanya mawasiliano na Waziri wa Afya Ummy Mwalimu ambaye tayari ameisha fanya mawasiliano na Mganga Mkuu wa Serikali ili kulichukua jambo hilo kwa haraka na kulifanyia uchunguzi wa kina ili kuleta matokeo kile kinachozungumzwa" alisema RC Chalamila.

Ameongeza kuwa hadi Sasa Mganga Mkuu wa Mkoa kwa Kushirikiana na Mganga Mkuu wa Serikali bado wanaendelea na uchunguzi na kuwa mara watakapokuwa tayari Wizara kupitia wataalam wa afya wataendelea na taratibu zao zitakavyowataka wafanye.

Aidha amesema kuwa hadi sasa bado hajaripotiwa mgonjwa yeyote aliyekwisha pata virusi au ugonjwa wa Ebola.

Hata hivyo Chalamila amewataka wananchi mkoani  humo kuendelea kuchukua tahadhari kama ilivyokuwa awali na kuwahimiza kuepuka taarifa hizi ambazo hazijatolewa na kuthibitishwa na wataalam wa afya badala yake wananchi wapuuze na kuendelee na shughuli zao za kiuchumi kwani Mkoa huo upo salama.

No comments:

Post a Comment

Pages