NA TULLO CHAMBO, RT
BAADA ya kumalizika kwa mashindano ya vijana chini ya miaka 18 na 20 Afrika Mashariki 'EAAR U 18&20 Championship' yaliyofanyika jijini Dar es Salaam Machi 10 na 11, Shirikisho la Riadha Tanzania (RT), sasa linajipanga kuelekea mashindano ya Afrika Lusaka Zambia.
Katika mashindano hayo ya Afrika Mashariki yaliyoshirikisha nchi sita, Tanzania Bara ilikamata nafasi ya tatu huku Kenya ikiibuka ya kwanza na Zanzibar ya pili.
Kwa mujibu wa Afisa Habari wa RT, Lwiza John, wanariadha na wadau mbalimbali wanaombwa kufanikisha ushiriki wa Tanzania kwenye mashindano hayo makubwa ya Afrika, kwa kuanzia mashindano hayo ya wazi ya Aprili Mosi.
"Tunawaomba vyama vya mikoa na wilaya, kusaidia kuwataarifu wanariadha walioko maeneo yao, ikiwemo vilabu na wadau mbalimbali kushiriki mashindano haya ya wazi yatakayofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa Aprili 1, ili tuweze kupata timu itakayokwenda kuipambania nchi huko Zambia," alisema Lwiza.
Lwiza, alisema mashindano hayo ni muhimu, kwani mbali na kutoa fursa kwa vijana wa umri huo kuonyesha vipaji vyao, yatatoa taswira ya ubora wa mchezaji kwa wakati husika.
Katika mashindano hayo ya Afrika, Tanzania Bara na Zanzibar zitaungana na kuunda timu moja itakayoshiriki mashindano hayo ya Afrika yanayotarajiwa kufanyika kuanzia Aprili 27 hadi Mei 3 mwaka huu.
No comments:
Post a Comment