March 25, 2023

Serikali kukagua shule Bukoba

 




Mkuu wa Wilaya ya Bukoba Yohana Siima akifunga mafunzo mbinu ya walimu kazini elimu ya awali kwa mfumo wa Montessori, mafunzo ambayo yalitolewa na chuo cha Partage kwa kushirikiana na serikali. Walimu waliohitimu ni 20 kutoka halmashauri nane za mkoa wa Kagera  na ifikapo mwaka 2025 wanarajia walimu 120 wawe wamemaliza masomo hayo.


Mkurugenzi Chuo cha Partage na shule ya Montasori Phllipe Krynen akizungumza katika mahafari ya kuhitimisha mafunzo mbinu ya walimu kazini elimu ya awali kwa mfumo wa Montasori yaliyofanyika jana katika ukumbi wa Bukoba  sekondari Manispaa ya Bukoba.


Na Alodia Babara, Bukoba


Mkuu wa Wilaya ya Bukoba mkoani Kagera Yohana Siima amesema atafanya ziara ya kukagua shule ili kuona mazingira wanayosomea wanafunzi kama ni rafiki kwao kupata elimu bora.


Siima aliyasema hayo Machi 24, mwaka huu akiwa mgeni rasmi kwa niaba ya mkuu wa mkoa wa Kagera katika mahafari ya kuhitimisha mafunzo mbinu ya walimu kazini wa kozi ya kwanza ya ualimu elimu ya awali kwa mfumo wa mentasori na walimu hao wapatao 20  wamemaliza masomo yao katika chuo cha Partage na walikuwa wanatoka shule za serikali katika halmashauri nane za mkoa wa Kagera.


Siima alisema kuwa, wanaweza kuwa wanaona wanafunzi wanapendeza barabarani kumbe huko wanakosomea mazingira yao si mazuri kwa ajili yao kupata elimu bora hivyo akasema atafika katika shule ya partage Montessori na shule nyingine zilizopo manispaa ya Bukoba ili aangalie mazingira wanayosomea wanafunzi  kama ni rafiki kwao kupata elimu bora.


“Nimeona hapa wanafunzi wakiwa na uwezo mzuri wa kuongea kiingereza lakini nitakagua shule zilizopo hapa manispaa ili kuona kule shuleni mazingira yakoje na kama ni rafiki kwa kujifunzia na kwa kupata elimu bora” amesema Siima.


Amesema ana imani kuwa  walimu waliohitimu jana elimu ya awali kupitia mafunzo ya miezi sita waliyoyapata wataweza kutatua changamoto mbalimbali na ilivyokuwa awali ikawe tofauti.


Aidha amesema ifikapo mwaka 2025 wanatarajia walimu 120 walioko kazini watakuwa wamepata mafunzo ya elimu ya awali na idadi hiyo itaongezeka iwapo walimu waliopata mafunzo watatekeleza yote waliyojifunza na aliwahimiza wazazi kuendelea kupeleka wanachuo wenye sifa za kujiunga na mafunzo hayo.


Naye mkurugenzi wa chuo cha Partage ambacho pia kuna shule ya Montessori Phillipe Krynen amesema mwaka 1990  walianzisha shule ya montasori na badae walianza kutoa mafunzo ya chuo cha ualimu elimu ya awali kama Partage  mwaka jana 2022 walianza  ushirikiano na serikali na mwezi Oktoba ndipo walimu 20 kutoka halmashauri nane za mkoa huo walianza mafunzo yao na kuhitimu jana.


Amesema wilaya ya Muleba walimu 4, Bukoba vijijini  3, Biharamlo 3, Karagwe 2, Kyerwa 2, Ngara 2, Misenyi 2 na manispaa ya Bukoba 2.


Kwa upande wake mthibiti ubora wa shule toka wizara ya elimu, sayansi na Teknolojia Mwl Augusta Lapokela amesema kuwa, wizara itaendelea kufuatilia na kusimamia elimu inayotolewa ngazi zote.


Mmoja wa wahitimu Edmond Dominick amesema kuwa, baada ya kupata masomo hayo wanaenda kuondoa changamoto zilizokuwepo na kuwafundisha kwa vitendo wanafunzi wa awali ili waweze kuelewa zaidi.

No comments:

Post a Comment

Pages