April 17, 2023

NMB yahitimisha uzinduzi kampeni ya miti kikanda kwa shangwe

 


Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora Dkt. John Mboya (kulia) akipokea moja ya mti kati ya 5,000 inayotarajiwa kupandwa mkoani humo kutoka kwa Afisa Mkuu wa Rasilimali  Watu NMB Emmanuel Akonaay, kwenye hafla ya upandaji miti kanda ya Magharibi iliyofanyika katika eneo la Magereza Kazima kata ya Ifucha.

 

Na Mwandishi Wetu

 

Benki ya NMB imehitimisha uzinduzi wa kampeni ya kupanda miti milioni moja nchi nzima kikanda wiki jana mkoani Tabora kwa ajili ya mikoa ya kanda yake ya magharibi kwa kupanda miti 5000 katika eneo la Gereza la Uyui.

 

Hafla hiyo ya mwisho katika kanda saba za benki hiyo ilifanyika Jumamosi na kuhudhuliwa na watu wengi ikiambatana na shamrashamra nyingi.

 

Kivutio kikubwa ulikuwa ni wimbo maalum wa umuhimu wa kupanda miti kutoka kwa vijana wa JKT Msange ambao mashairi yake yalimvutia kila mtu aliyeshiriki kwenye shughuli hiyo katika Kambi ya Magereza - Kazima.

 

Wakicheza kwa madaha na mbwembwe, vijana hao walishangiliwa kwa vigeregere na nderemo huku wanawake wajasiriamali wa Manispaa ya Tabora wakiipamba pia hafla hiyo kwa namna ya kipekee kabisa.

 

Kiongozi wao, Bi Ashura Shaban Mwazembe, alisema shangwe lao lilitokana na kuguswa na jinsi Benki ya NMB ilivyojitolea kuikijanisha Tabora na Tanzania nzima kwa ujumla.

 

Mbali na viongozi wa mkoa, wilaya na manispaa, zoezi la kupanda miti 5000 siku hiyo pia liliwashirikisha wananchi wa Kata ya Ifucha, maafisa wa vyombo vya ulinzi na usalama, watumish wa umma, wakereketwa wa mazingira na wanafunzi wa shule mbili za msingi katika kata hiyo.

 

Mgeni rasmi alikuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Tabora (RAS), Dkt. John Rogath Mboya, aliyemwakilisha Mkuu wa Mkoa, Balozi Dkt. Batilda Burhan.

 

Pia walikuwepo watendaji wa Mamlaka ya Huduma za Misitu Tanzania (TFS).

Taasisi hiyo ndiyo  inayoratibu zoezi zima la mradi wa NMB wa kuikijanisha Tanzania.

 

Ujumbe wa NMB inayoendesha kampeni hiyo kama sehemu ya ajenda yake ya uendelevu uliongozwa na Afisa Mkuu wa Rasilimali Watu, Bw Emmanuel Akonaay.

 

Miongoni mwa vitu alivyovibainisha Bw Akonaay ni kwamba mwaka huu wameongeza TZS bilioni 2 kwenye bajeti ya kuwajibika kwa jamii (CSR) hadi TZS bilioni 6.2 kwa ajili ya kufadhili michakato ya maendeleo endelevu.

 

Ongezeko hilo ndilo NMB inalolitumia kufadhili kampeni ya kupanda miti milioni moja ambao ni uwekezaji uliopongezwa sana na wakazi wa Tabora.

 

“Kupanda miti mipya milioni moja ni jambo kubwa na la heri si tu kwa mkoa wetu na kanda hii bali pia kwa nchi nzima na dunia yote kwa ujumla. Huu ni mchango muhimu katika harakati za kulikabili janga la athari za tabia nchi,” Dkt Mboya alibainisha..

 

“Ni wajibu wetu sisi wote na kama taifa kuziunga mkono taasisi kama NMB zinazoupa utunzaji mazingira kipaumbele,” alisisitiza.

 

Dkt Mboya aliitaja NMB kama mfano wa kuigwa kwa kuitikia haraka wito wa Rais Dkt Samia wa upandaji miti kuwa zoezi endelevu na sehemu ya maisha ya kila Mtanzania.

 

Kwa mujibu wa Bw Akonaay, lengo la NMB ni kupanda miti 250,000 katika kanda ya Magharibi ambayo ardhi yake inauwezo mkubwa sana wa kuotesha miti asili katika kipindi hiki cha kampeni yao ambayo kitaifa ilizinduliwa Machi 27 jijini Dodoma na Makamu wa Rais, Dkt Philip Mpango.

 

Baada ya uzinduzi huo jijini Dodoma, NMB imekuwa ikifanya uzinduzi kikanda zoezi lilioanzia Zanzibar Machi 28..

 

Bw Akonaay alisema mbinu nyingine ya kuhakikisha ufanisi wa kampeni hiyo ni ushirikishwaji wa wanafunzi kupitia shindano la upandaji miti mashuleni la “Kuza Mti Tukutuze”.

 

Thamani ya shindano hilo ni TZS milioni 472 na lengo lake ni kuhakikisha miti itakayopandwa inakua na kuleta matokeo chanya. Washindi wake watangazwa mwezi Juni mwaka 2024 huku zawadi tatu za kwanza zikiwa ni pesa taslimu TZS milioni 50, 30 na 20..

 

“Shindano hili pamoja na kuhimiza upandaji miti linalenga pia kutoa elimu na kuongeza uelewa wa umuhimu wa kutunza na kulinda mazingira kwa wanafunzi na vijana ambao ni vizazi vyetu vya kesho,” Bw Akonaay alifafanua.


No comments:

Post a Comment

Pages