HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 06, 2023

AWESO AENDELEZA JITIHADA ZA UPATIKANAJI WA MAJI JIJI LA DODOMA

Waziri wa Maji Mhe. Jumaa Aweso amekagua maendeleo na kupokea mabomba kwa ajili ya mradi wa maji Nzuguni jijini Dodoma ambapo amesema mradi huu ni wa haraka na utendaji wake ni wa tofauti na fedha zake zitoke kwa haraka kwani wananchi wanataka maji. 

Aweso amesema, Baada ya kubainika uwepo wa Bonde lenye maji mengi ukanda wa Nzuguni DUWASA imechimba visima vitano (5) vyenye uwezo wa kuzalisha lita milioni 7.6 kwa siku. Maji yaliyopatikana yataongeza uzalisha kutoka lita million 68.6 hadi 76.2 kwa siku, sawa na ongezeko la asilimia 11.7 kutoka kwenye uzalisha wa sasa. Mradi huu utawanufaisha wananchi wa Nzuguni, Kisasa, Ilazo na Swasawa.

Amefafanua kuwa kwakuwa mabomba yamefika ni vyema kisiwepo kisingizio cha mkandarasi kukosa fedha ili mradi ukamilike kwa wakati uliopangwa.



Aidha, amemwagiza Mkurugenzi wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (DUWASA) Mhandisi Aron Joseph ahakikishe vifaa vinafika kwa wakati ili mabomba hayo yasambazwe na wananchi wapate huduma ya maji haraka.
Vilevile, ameishauri timu ya Rasilimali za Maji kufanya utafiti wa ziada ili kupata maeneo mengine yenye maji ya kutosha pembezoni mwa jiji la Dodoma ili visima viongezwe na wananchi wapate huduma hiyo kwa urahisi.


Pia, Waziri Aweso amesisitiza kuwa katika kipindi chote cha utekekezaji wa mradi wizara itasimamia ili wananchi wapate maji na atakua mguu kwa mguu kufuatilia hilo.

Aidha, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maji Mhandisi Nadhifa Kemikimba amesema watahakikisha fedha zinatolewa kwa wakati mara baada ya mkandarasi kupeleka malipo anayotakiwa kupewa.

Katika hatua nyingine, Mkurugenzi Mkuu DUWASA Mhandisi Joseph amesema utekelezaji wa mradi huo katika Kata ya Nzuguni utakaonufaisha wakazi 75, 968 unatarajiwa kukamilika Agosti mwaka huu akifafanua kuwa mradi huo wenye mikataba minne yenye thamani ya sh. Bilioni 4.8 ambapo hadi sasa DUWASA imepokea sh. 1.08 bn ambazo ni 100% ya malipo ya awali kwa wakandarasi wote.

No comments:

Post a Comment

Pages