HABARI MSETO (HEADER)


Breaking

May 06, 2023

BIASHARA KATI YA TANZANIA NA UFARANSA YAONGEZEKA

Ukuaji wa biashara kati ya Tanzania na Ufaransa umeongezeka kutoka kiasi cha shilingi billioni 27.8 kwa mwaka 2015 hadi bilioni 94.5 kwa mwaka 2022.

 

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Mhe. Dkt. Stergomena Tax (Mb.) amebainisha hayo alipofungua mkutano wa pili wa majadiliano ya kidiplomasia kati ya Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Serikali ya Ufaransa uliofanyika Jijini Dar es Salaam.

 

Mbali na kukua kwa biashara kati ya mataifa hayo mawili, pia kumekuwa na ongezeko la watalii kutoka Ufaransa ambapo kwa mwaka 2022 Tanzania ilipokea watalii 100,600 kutoka Ufaransa na kuwa nchi ya pili kuleta watalii nchini Tanzania.

 

“Biashara imeendelea kukua lakini pia katika uwekezaji tunashirikiana, katika utalii Ufaransa imekuwa nchi ya pili kwa kuleta watalii kwenye taifa letu, haya yanatokana na juhudi mbalimbali zinazofanywa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Mheshimiwa Dkt. Samia Suluhu Hassan. Serikali imefanya kazi kubwa kuvutia wawekezaji na watalii hususan kupitia filamu ya ‘Royal Tour’ na ndiyo maana utalii umeongezeka,” alisema Dkt. Tax

 

Mhe. Dkt. Tax amesema madhumuni ya mkutano huu wa majadiliano ambao ni wa pili kati ya Tanzania na Ufaransa ni kuwawezesha Wafaransa kutambua fursa mbalimbali zinazopatikana nchini pamoja na Watanzania kuzijua fursa zinazopatikana nchini Ufaransa ili kuzitumia kwa maslahi ya pande zote mbili.

 

“Tanzania na Ufaransa zimekuwa zikishirikiana katika sekta za elimu, nishati, utalii, usafirishaji, ulinzi na usalama (maritime security) …...Ufansa wamekuwa wadau wakubwa katika ujenzi wa bomba la mafuta linalojengwa kutoka Uganda hadi Tanzania mambo yote haya lazima tuendelee kuyadumisha lakini pia kufungua fursa nyingine zinazoweza kupatikana,” alisisitiza Dkt. Tax

 

Naye Balozi wa Ufaransa nchini, Mhe. Nabil Hajlaoui amesema kufanyika kwa mkutano huo wa pili wa majadiliano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Ufaransa ni uthibitisho kuwa Tanzania na Ufaransa zimekuwa na ushirikiano mzuri na imara.

 

“Tumekuwa tukikutana mara kwa mara na kujadili masuala ya kikanda na kimataifa ili kuimarisha maendeleo ya miradi kati ya nchi zetu mbili katika sekta mbalimbali hususan mabadiliko ya tabianchi, uwekezaji, utalii, uchumi wa buluu, usalama wa baharini, na tumefanikiwa kujadili masuala yote vizuri kwa sababu uhusiano mzuri tulio nao. Itakumbukwa kuwa mwaka jana 2022 Marais wetu walipokutana na walikubaliana kushirikiana na kusonga mbele kwa maslahi ya pande zote mbili,” alisema Balozi Nabil.

 

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu Idara ya Afrika kutoka Wizara ya Ulaya na Mambo ya Nje ya Ufaransa, Bw. Christophe Bigot amesema Ufaransa itaendelea kushirikiana na Tanzania katika kukuza na kuimarisha sekta za biashara na uwekezaji, nishati, usalama wa baharini, uwekezaji, utalii, uchumi wa buluu, michezo na utamaduni.

 

Mkutano huo pia umehudhuriwa na Makatibu Wakuu na Manaibu makatibu Wakuu kutoka Wizara mbalimbali wakiongozwa na Katibu Mkuu Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt. Samwel Shelukindo, Kituo cha Taifa cha Uwekezaji (TIC) na Mamlaka ya Uwekezaji Zanzibar (ZIPA).

 

Mkutano wa kwanza wa majadiliano ya kidiplomasia kati ya Tanzania na Ufaransa ulifanyika mwezi Juni 2018 nchini Ufaransa.

No comments:

Post a Comment

Pages