May 05, 2023

GEAY 'AKICHAFUA' MBEYA TULIA MARATHON 2023

BINGWA wa Taifa anayeshikilia rekodi ya Marathon Tanzania, Gabriel Gray amekuwa kivutio kikubwa Mbeya Tulia Marathon, aliposhiriki na kuibuka mshindi katika mbio za mita 1500.
Mbeya Tulia Marathon, imekata utepe Leo Mei 5 kwa mbio za uwanjani, kabla ya kesho Jumamosi Mei 6 kurindima Marathon.

Katika mbio hizo za mita 1500, Geay alianza taratibu raundi ya kwanza akiwa nyuma, kabla ya mzunguko wa pili kupata dhoruba la kuangushwa, lakini alinyanyuka na kukiwasha na hatimaye kuibuka mshindi akitumia dakika 3:58.46.


Geay alifuatiwa na Faraja Damas wa JWTZ aliyetumia dakika 4:00.08 huku nafasi ya tatu ikienda kwa John Joseph pia JWTZ 4:06.25. 


Mashabiki na viongozi mbalimbali waliojitokeza, wakiongozwa na Mkuu wa Wilaya ya Mbeya, Beno Malisa, walishindwa kujizua kumshangilia Geay wakati akikiwasha katika mbio hizo.


Kwa upande wa wanawake Mita 1500, Magdalena Shauri wa JWTZ, alishinda akitumia dakika 4:31.13 na kufuatiwa na Salma Charles ambaye katoka Zambia na Timu ya Taifa U 18 na 20 iliyoshiriki mashindano ya Afrika, dakika 4:46.55 na wa tatu akiwa ni Mayselina Mbua JWTZ 4:53.16.


Mbali na Geay ambaye katoka kufanya kweli katika mbio kongwe za Boston Marathon nchini Marekani alikoshika nafasi ya pili hivi karibuni, pia mkali mwingine, ambaye pia ni Mshindi wa medali ya Fedha Jumuiya na Mwanamichezo Bora Tuzo za BMT 2022, Alphonce Simbu, naye alikuwepo kushuhudia mbio hizo.


Pia, Timu ya Taifa ya Vijana iliyopumzika hapa ikitokea Ndola Zambia ilikojinyakulia medali mbili katika mashindano ya Afrika, baadhi walipata nafasi ya kushiriki mbio za uwanjani Mbeya Tulia Marathon.


Timu hiyo inatarajiwa kuondoka Mbeya kesho Jumapili kurejea Dar es Salaam.


Pia, mbio hizo zilipambwa program ya watoto 'Kids Athletics', ambayo ilikuwa kivutio kwa watoto wa shule za msingi walioshiriki.

No comments:

Post a Comment

Pages