Meneja wa Chama cha ushirika cha Msingi Mkombozi Alphonce Vedasto akizungumza katika mkutano huo.
Na Lydia Lugakila, Kyerwa.
Chama cha ushirika cha Msingi Cha Kilimo Hai na Soko la haki kinachozalisha Kahawa ya Maganda Wilaya Kyerwa Mkoani Kagera kimepongezwa na Halmashauri ya Wilaya hiyo, kutokana na kutekeleza Maagizo ya Serikali, ikiwemo pia maelekezo ya Baraza la madiwani la Halmashauri hiyo lililoweka mpango na mkakati wa kuagiza AMCOS zote zilizo tayari kujenga Viwanda Wilayani humo.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Mwaka 2023/2024, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kyerwa, Bahati Henerco ambaye amekuwa Mgeni rasmi amesema kuwa ni jambo la kujivunia katika Wilaya hiyo, kutokana na Agizo la Serikali kutekelezwa, kwani licha ya kiwanda hicho Mkombozi kufanikiwa pakubwa, kimewawezesha Wakulima wa Kahawa kuwa wanufaika wa zao hilo.
"Kyerwa tuna Viwanda vitatu vinavyokoboa Kahawa tunawashukuru Mkombozi na wengineo, kwa hatua hii pia tunamshukuru Rais Dokta Samia, kwa anavyowapigania Watanzania, hivyo tujue wajibu wetu na kutumia fursa hizo, ili zituwezeshe kiuchumi" alisema Henerco.
Kupitia Viwanda hivyo amewasihi Wakulima kuweka jitihada katika kilimo, kutokana Wilaya hiyo kugawa miche mingi ya Kahawa,ili kuboresha zao hilo.
Aidha amewahimiza Wananchi Wilayani humo kujiunga katika AMCOS ili kuhakikisha Kahawa hiyo inauzwa kwa njia ya mnada.
Aidha akizungumzia Kiwanda hicho na hatua zake, Mwenyekiti wa Chama cha ushirika cha Msingi Mkombozi Wilbard Edward amesema kiwanda
kina thamani ya Shilingi Bilioni 2.9 na kina uwezo wa kukoboa tani 6 kwa saa.
"Malengo yetu ni kuweka huduma karibu, kuendelea kuboresha zao la Kawaha katika Wilaya hii,ili kumnufaisha Mkulima na kuongeza mapato katika Halmashauri na Taifa kwa ujumla" alisema Wilbard.
Naye Meneja wa Chama cha ushirika cha Msingi Mkombozi, Alphonce Vedasto Nkesiza, amesema wataendelea kusimamia ubora, kuongeza wanachama na kupanua wingo kwa kushirikiana na Serikali na wadau wa Maendeleo.
Aidha kwa upande wao wakulima wa Kahawa na wanachama wa Chama hicho akiwemo Gilidius Dauson, Ndibalema Cronery na Seleman Mussa wameiomba Serikali kuona namna ya kuwa inawakopesha mikopo kabla ya msimu, ili waweze kuboresha mashamba yao, huku wakidai kucheleweshewa malipo yao na kujikuta wamekwama katika kukidhi mahitaji yao.
Akijibu juu ya kucheleweshewa malipo ya baadhi ya wakulima Mjumbe wa Bodi hiyo Bi Mektrida John amesema changamoto zinazotokana na Wakulima wenyewe kupima Kahawa kwa kutumia mtu mwingine, huku akidai kuwa Makalani wa Vijijini wamekuwa Changamoto kwani wanapokusanya Kahawa wanawapimia Wakulima bila kuwaingiza kwenye vitabu.
No comments:
Post a Comment