May 03, 2023

TanTrade yapendekeza mkataba wa ruzuku za uvuvi wa WTO uzingatie wafanyabiashara na Wavuvi wadogowadogo


Na Mwandishi Wetu 


MAMLAKA ya Maendeleo ya Biashara Tanzania (TanTrade) imependekeza mkataba wa ruzuku na uvuvi wa Shirika la Biashara Duniani (WTO) uzingatie Wafanyabiashara na wavuvi wadogo wadogo.



Hayo yamebanishwa hivi karibuni na Mkurugenzi wa Idara ya Uendelezaji Biashara TanTrade, Freddy Liundi wakati warsha iliyoandaliwa na WTO kwa lengo la kujenga uelewa kuhusu sekta ya uvuvi kwa wadau mbalimbali kutoka Afrika Kusini, Kenya, Uganda, Tanzania, Lesotho na Misri.



Liundi amesema TanTrade inapongeza jitihada zinazofanywa na WTO katika kutunza rasimali za bahari na inaendelea kushirikiana na shirika hilo katika kutoa ushauri wa kisera unaozingatia ustawi wa wafanyabiashara na wavuvi wadogogo nchini.



Awali akifungua warsha hiyo Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Uchumi wa Buluu na Uvuvi, Zanzibar, Khamis  Mwalimu amesema ni muhimu mkataba huo kutoa nafasi ya kisera kwa nchi zinazoendelea kwa kuzipatia upendeleo maalum ili Serikali ziweze kuendeleza sekta ya uvuvi na rasilimali hai zilizoko baharini.


 


Mwalimu amesema kuwa sekta ya uvuvi inamchango mkubwa kwa uchumi wa bara la Afrika ambapo kwa Tanzania ina kilometa 223 za eneo la uvuvi katika bahari ya hindi ambazo zimetoa ajira, hifadhi ya chakula, kipato kwa watu na Serikali hivyo ni muhimu mkataba huo ukazingatia mahitaji hayo.


 


Kwa upande wake Naibu Katibu Mkuu wa WTO, Angella Ellard ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kuandaa warsha hiyo na kwa ushirikiano mzuri na


kusema kuwa jambo lililofanyika ni muhimu ya kwakuwa bahari inakabiliwa na changamoto nyingi, ikiwa ni pamoja na kupungua kwa idadi ya samaki ambayo inaendelea kila kukicha. 



Amesema serikali nyingi zinaendelea kutoa ruzuku za uvuvi bila kuzingatia athari zake kwa ustahimilivu na kuongeza kuwa ruzuku hizo zinakadiriwa kufikia dola Bilioni 35 kwa mwaka ulimwenguni, ambapo dola bilioni 22 zinahusiana na kuongeza uwezo wa uvuvi.



"Ruzuku hizo zinafanya meli nyingi za uvuvi kufanya kazi kwa muda mrefu baharini na kusababisha athari kwa mazingira na rasilimali za bahari," amesema Ellard



Mkataba wa kudhibiti ruzuku sekta ya uvuvi umejadiliwa takribani miaka 20 kabla ya nchi wanachama wa WTO kufikia  makubaliano ya awali Juni 2022 wakati wa mkutano wa 12 wa WTO wa mawaziri unaofahamika kama Twelfth Ministerial Conference -MC12 wenye lengo la kulinda uendelevu wa rasilimali hai zilizopo baharini hususan samaki kupitia kudhibiti ruzuku ambazo zinasabanisha wavuvi kuwa na uwezo mkubwa wa kuzunguka bahari zote na kufanya uvuvi usio endelevu.


Awamu ya pili ya majadiliano ya kuhitimisha mkataba huo yanaendelea ambapo masuala muhimu yanayotarajiwa kujadiliwa ni pamoja na kuhakikisha mkataba huo unajumuisha upendeleo  maalum kwa nchi zinazoendelea na wavuvi wadogo na yanatarajiwa kukamilika kabla ya mkutano wa 13 wa WTO wa Mawaziri (MC13) utakaofanyika Fenruari 2024.


No comments:

Post a Comment

Pages