May 18, 2023

Walinda amani wa UN kutoka Tanzania wapokea pongezi kutoka JWTZ, MINUSCA


Brigedia Jenerali George Itangare, akikagua Kikosi cha Sita cha Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania (TANBAT6) kilichopo eneo la Nola Wilaya ya Beriberati Mambele Kadei
Afrika ya Kati mara alipotembea kikosi hicho kujua utayari wake (Picha na Kapteni Mwijage Inyoma).

 

Na Mwandishi Wetu


JESHI la Ulinzi wa Wananchi Tanzania (JWTZ) limewapongeza walinda amani Kikosi cha sita cha Umoja wa Mataifa kutoka Tanzania (TANBAT 06) kwa namna wanavyofanyakazi kwa bidii huku wakiwataka kuzingatia maadili ili wasiuchafue umoja huo.


Walinda amani hao ambao wanaohudumu chini ya ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kulinda amani nchini Jamhuri ya Afrika ya Kati (MINUSCA) wamepokea pongezi hìzo wakati  ugeni na salamu kutoka JWTZ kupitia ujumbe uliongozwa na Brigedia Jenerali George Itang’are aliyewakilisha salamu za Mkuu wa Majeshi ya Tanzania.


Akizungumza wakati akiwasilisha salamu hizo jana mjini Berbérati mkoani Mambere Kadei Afrika ya Kati, Brigedia Jenerali Itang’are alisema ni muhimu kwa walinda amani hao kuzingatia maadili ili wasiuchafue Umoja wa Mataifa, Jeshi la Tanzania na taifa lao kwa ujumla.


"Hakika mnafanya kazi kubwa na nzuri hivyo pokeeni salamu za pongezi, tunawaomba mzingatie maadili ili msije kulichafua jeshi letu la Tanzania, taifa leo na Umoja wa Mataifa (UN) kwa ujumla," alisema

 

Naye Mwambata Jeshi katika Uwakilishi wa kudumu wa Tanzania kwenye Umoja wa Mataifa (UN), Brigedia Jenerali Robert Mtafungwa alisema kuwa lengo la ziara ya ujumbe huo ni kuangalia utayari wa kikosi lakini pia kuwapongeza kwa kazi nzuri wanayofanya walinda amani hao pale wanapopewa jukumu. 


Kwa upande wake Mkuu wa TANBAT 06 Luteni Kanali Amini  Mshana alilishukuru Jeshi la Tanzania kufanya ziara ya kutembelea kikosi hicho nchini Afrika ya Kati na kuwatia.moyo wa kuendelea kufanya kazi.


Aidha aliwakumbusha askari kuwa yaliyozungumzwa yatafanyiwa kazi na kwamba ameahidi  kuendeleza mafanikio waliyoyaona ikiwemo kutekeleza maelekezo ambayo wameyapokea.

No comments:

Post a Comment

Pages