Balozi wa China nchini Tanzania Chen Mingjian akizungumza katika ufunguzi wa kongamano la kusherehekea miaka 10 ya BRI.
Naibu Spika wa Bunge la Tanzania Mussa Zungu akifungua kongamano la kusherehekea miaka 10 ya BRI.Mwenyekiti wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph Butiku akizungumza kwenye kongamano la kusherehekea miaka 10 ya BRI.
Na Mwandishi Wetu
NCHI
ya China imesema ukuaji wa biashara kati yake Tanzania kuanzia mwaka
2022 hadi Juni, 2023, umefikia Dola za Marekani bilioni 8.31 sawa na
shilingi trilioni 20 za Kitanzania, ikiwa ni zaidi ya mara tatu na nusu
ya muongo uliopita.
Aidha
mataifa hayo yamezidi kuimarisha uhusiano ndani ya miaka 10 ya
kutekelezwa kwa Mpango wa Ukanda Mmoja, Njia Moja (BRI), unaoratibiwa na
China ambao umefungua fursa nyingi za biashara baina ya wananchi wa
mataifa hayo.
Alisema
manufaa ya BRI nchini, yamekuwa na mchango mkubwa katika kukuza
biashara ya nchi hizo hivyo ni imani yake kubwa mafanikio yataongezeka.
Tanzania
ni miongoni mwa mataifa 52 ya Afrika yaliyoridhia BRI ambayo inatimiza
miaka 10 hasa kwenye ujenzi wa miundombinu muhimu katika kuchochea
maendeleo.
Balozi
Mingjian alisema uhusiano baina ya Tanzania na China ndani ya miaka 10
sasa ya kutekelezwa kwa mpango wa BRI umezidi kuimarika na kujengeka
ambapo biashara baina yetu na imefikia Dola za Marekani bilioni
8.31,hii ni ukuaji wa wa zaidi ya maratatu na nusu ukilinganisha na
kipindi cha miaka 10 iliyopita.
Alisema
bidhaa za Tanzania zilizoingia kwenye soko la China zimeongezeka
ikiwemo soya, parachichi na nyingine nyingi zimeshaingia kwenye soko
hilo na zinaendelea kufanya vizuri.
Alisema
kupitia mpango wa BRI, uwekezaji wa China nchini Tanzania umeongezeka
ambapo sasa taifa hilo ndilo linaongoza kwa uwekezaji wa miradi mikubwa
ikiwa ni mara mbili na nusu ya miaka 10 iliyopita.
"Miradi
mikubwa ya maendeleo mfano ya ujenzi wa reli ya kisasa nchini Tanzania
vinatekelezwa na kampuni za China ikiwemo ya Reli ya SRG, Bwawa la
Kuzalisha Umeme la Mwalimu Nyerere (NJHPP), Bomba la Mafuta kutoka
Uganda kuelekea Tanga, Mkongo wa Taifa na miradi mingine
mikubwa,"alisema.
Alisema
pia Tanzania imenufaika na fursa za ufadhili wa masomo ambapo zaidi ya
wanafunzi 2,000 wa Kitanzania wamenufaika nazo huku pia taifa
likinufaika na ujenzi wa vyuo vya ufundi stadi vilivyojengwa kwenye
maeneo tofauti nchini.
Aidha,
alisema maktaba kuu ya UDSM, imejengwa kwa ufadhili wa watu wa China na
kuwa fursa nyingine lukuki zimetolewa kwa Watanzania vijana kuongeza
ujuzi na maarifa katika maendeleo ya teknolojia na hiyo ni matokeo
chanya ya kutekelezwa kwa mpango wa BRI nchini.
Akifungua
kongamano hilo, Naibu Spika wa Tanzania Mussa Hassan alisema Mpango wa
BRI kwa Tanzania umefungua fursa nyingi za maendeleo na kuimarisha zaidi
uhusiano baina ya Tanzania na China.
Alisema
China imeendelea kuwa rafiki na mdau muhimu wa maendeleo kwa mataifa ya
Afrika hususan katika kusaidia utekelezaji wa miradi mikubwa kama ya
ujenzi wa miundombinu na hiyo imesaidia kuunganisha mataifa ya Afrika
zikiwemo nchi za Afrika Mashariki kwa barabara za lami.
Zungu
alisema ushirikiano wa Tanzania na China unapaswa kuendelezwa kwa kuwa
una lengo la kuchochea maendeleo na sio manufaa ya upande mmoja.
"China
ina mchango mkubwa kwenye maendeleo ya Tanzania, hivyo tunapaswa
kutumia BRI kuhakikisha tunafika huko ilipo kwani ni wazi mpango huu una
faida kwa jamii zetu sisi wa nchi zinazoendelea,"alisema.
Mwenyekiti
wa Bodi ya Wadhamini ya Taasisi ya Mwalimu Nyerere (MNF), Joseph
Butiku akizungumza kwenye kongamano hilo alisema Tanzania na nchi za
Afrika zimenufaika na mpango wa BRI katika eneo la amani, umoja na
maendeleo.
Alisema
mpango huo ambao umesaidia kuboresha miradi mbalimbali ya maendeleo
ikiwemo miundombinu mikubwa ya ujenzi kama ya reli ya kisasa ambazo
zitaunganisha mataifa ya Afrika Mashariki.
“Taasisi
ya Mwalimu Nyerere tunaridhishwa na ushirikiano baina ya China na
Tanzania, wamekuwa rafiki wakubwa kwa taifa letu, tangu enzi za kiongozi
wa taifa hilo Mao Zedong na Mwalimu Nyerere hadi leo, naamini tukiamua
kuitumia BRI kama Wachina wanavyotaka tutafika mbali,”alisema Butiku.
Mwenyekiti
huyo alisema Afrika inapaswa kuitumia China kwa usahihi kwa kuwa
inataka nchi zote kuendelea kwa pamoja na sio kunyonya kama zingine
zinavyofanya.
"China
inatamani nchi kuendelea sio kutawala wengine, wao wanatafuta
ushirikiano na kufanya biashara ni masuala ya amani,umoja na
maendeleo,"alisema.
Naye
Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Mapinduzi (CCM), Richard
Kasesera amewataka Watanzania kutumia fursa za kiuchumi zinazopatikana
China kwa faida.
"China
inahitaji mazao mbalimbali kutoka Tanzania kama Muhogo na mengine,
nadhani tunapaswa kulima kwa nguvu zote ili tuweze kunufaika na soko
hilo,"alisema.
Mbunge
wa zamani wa Jimbo la Mwibara wilayani Bunda mkoani Mara Muttamwega
Mgaywa alisema Tanzania inapaswa kukuza na kuendeleza ujuzi ambao
unapatikana China ili kuhakikisha uzalishaji wa bidhaa unafanyika hapa
nchini.
Mgaywa alisema mafanikio ya China yamechangiwa na uthubutu, hivyo ni jukumu la Tanzania na nchi za Afrika kuishi mfano huo.
Waziri
wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi mstaafu, Profesa Anna Tibaijuka
alisema BRI ni njia sahihi ya kuzifanya nchi za Afrika kufikia malengo,
hivyo ni jukumu la viongozi kuisimamia kwa nguvu kubwa.
Mpango
wa BRI ulianzishwa China mwaka 2013 kusaidia mataifa mbalimbali katika
bara la Asia, Afrika na Ulaya ambapo zaidi ya nchi 150 zimenufaika na
uwekezaji wa zaidi ya Dola za Marekani trilioni moja, huku miradi
mbalimbali ya ushirikiano 3,000 ikitekelezwa na ajira zaidi ya 420,000
zikitolewa katika nchi zilizojiunga na mpango huo.
Aidha
mpango huo umesaidia takribani watu milioni 40 kuondoka kwenye umaskini
uliokithiri katika mataifa hayo yaliyojiunga na BRI.






No comments:
Post a Comment