Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika Amath Pathe.
Na Selemani Msuya
MKURUGENZI Mkuu wa Mkuu wa Jukwaa la Mifumo ya Chakula Afrika (AFS Forum), Amath Pathe amesema mkutano uliofanyika hapa nchini kuanzia Septemba 5 hadi 8, 2023 umeweka rekodi kwa kuhudhuriwa na washiriki zaidi ya 5,400 maraisi watano na mawaziri kutoka nchi 90 duniani.
Pathe, amesema hayo leo wakati wa kufunga jukwaa hilo na kutangaza kuwa lijalo litafanyika nchini Rwanda mwaka 2024, ambapo amepongeza Watanzania kwa kuwa na upendo.
"Hii ni namba kubwa ya washiriki katika jukwaa hili tangu lianzishwe, limeonesha ni namna gani nchi za Afrika zimedhamiria kuchukua hatua kuhusu mifumo ya chakula, kusema kweli nimpongeza Rais Samia Suluhu Hassan na wasaidizi wake kwa kuandaa mkutano huu ambao umefana," amesema.
Amesema majadiliano katika AFS yameonesha dhahiri kuwa ushirikiano kati ya Serikali, wafanyabishara, asasi za kiraia, wakulima, taasisi za kitafiti na mashirika mbalimbali utatengeneza misingi endelevu ya mifumo ya chakula Afrika.
Pathe amesema siku nne za jukwaa hilo zimewezesha taasisi mbalimbali kukubali kuwekeza katika miradi mbalimbali ambayo itahusisha vijana na wanawake.
Kwa upande wake Waziri wa Kilimo Hussein Bashe, Serikali imepanga kuwaingiza vijana na wakina mama katika kichocheo cha kuleta mapinduzi ya mifumo ya chakula.
Waziri Bashe amesema sekta binafsi ni nguzo muhimu katika uwekezaji kwenye sekta ya kilimo na kwamba watawaunga mkono wakati wowote.
"Wakulima wadogo wa Afrika hawahitaji msaada wa mashirika ya maendeleo, bali wanahitaji haki zao katika mifumo ya dunia," amesema.
Aidha, Bashe ameweka wazi kuwa Jukwaa la AFS limewezesha Tanzania kupata fedha zaidi ya shilingi trilioni 1 kwa ajili ya kukuza na kuendeleza kilimo.
No comments:
Post a Comment