September 06, 2023

Bashe atangaza neema kwa wakulima nchni

Na Selemani Msuya
 
WAZIRI wa Kilimo Hussein Bashe amesema mradi wa kuchimba visima 67,500 na wa kumpatia kila mkulima hekari 2.5 za umwagiliaji bure na tenki la lita 5000 ni moja ya jitihada za kuhakikisha mkulima anapata urahisi wa kufanya kilimo.
 
Waziri Bashe aliyasema hayo jana jijini Dar es Salaam wakati wa mjadala wa afya ya udongo katika kilimo uliyofanyika kwenye  Mkutano wa siku nne wa Mifumo ya Chakula Afrika (AGRF 2023) unaoendelea jijini Dar es Salaam katika Ukumbi wa Kimataifa wa Mwalimu Nyerere (JNICC).

 
Alisema pia wana programu za kufikia hekari Milioni 8.5 za umwagiliaji hadi kufikia 2030 na kwamba kwa mwaka jana walikuwa na hekari 720,000.
 
Alisema ili kufanikisha yote hayo wanahitaji wastani wa Sh. Trilioni 1.3 kwa mwaka hivyo katika mkutano huo wa AGRF Rais ameweza kuwasaidia kama nchi kuweza kupata mradi wa Dola za Marekani Milioni 300 kwa ajili ya umwagiliaji kwenda kwenye kilimo.
 
“Pia tutazindua mradi na Benki ya Maendeleo ya Afrika ambao utaanza Januari mwaka kesho wa Dola za Marekani Milioni 100 kwa ajili ya kwenda kwenye kilimo na unawahusu vijana wa nchi hii, kwahiyo lengo la mkutano huu ni kuionesha dunia rasilimali zilizopo nchini na kwa namna gani watanzania watashiriki  kuzitumia ili tuweze kufanya biashara na wenzetu duniani hasa ya chakula,” alisema.
 
Akizungumza katika mjadala huo kuhusu afya ya udongo, Mtaalamu wa Masuala ya Udongo kutoka Taasisi ya Alliance Biodiversity International, David Guerena ameishauri serikali kushirikiana nao ili kutatua changamoto zinazoathiri ubora wa mazao na kuvutia vijana wengi kushiriki katika uzalishaji.
 
Alisema vijana wengi wanaojikita katika kilimo wanakatishwa tamaa na kutokuwa na tija katika uzalishaji huo kunakotokana na changamoto mbalimbali ikiwamo afya ya udongo na mbegu.
 
Guerena alisema watafiti wanafanya kazi kubwa ya kuboresha mnyororo wa thamani wa mazao ya kilimo kama vile mbegu bora na virutubisho vya kuweka kwenye udongo ili kutoa mazao bora, vitu ambavyo vinakatisha tamaa vijana kushiriki katika kilimo.
 
“Tanzania kuna vijana wengi  wanaotoka vijijini kwenye ardhi ya kutosha kulima lakini wanaishi bila ya ajira licha ya kuwa na elimu, ujuzi na nguvu za kufanya kazi, kwa hiyo tukiweza kufanya kazi pamoja na serikali na mashirika binafsi tunaweza kusaidia vijana kwenda mashambani wakiwa na ujuzi wa kutosha kwa hiyo tunahitaji  kusaidiana, ” alisema Guerena
 
Alisema kwa muda waliofanya utafiti katika kilimo hapa nchini wamegundua afya dhofu ya udongo ni moja ya sababu kubwa zinazopunguza tija kwenye mazao ya kilimo na kusababisha vijana kukimbia kilimo ikiwamo maeneo ya  kusini mwa nchi kama vile Iringa, Songwe na Mbeya na kanda ya ziwa ikiwamo Bukoba, Kagera.
 
Naye Mkurugenzi wa Ushirikiano wa Kimkakati kutoka taasisi ya utafiti wa mazao ya YARA International, Oystein Botillen, alisema katika kukabiliana na changamoto ya udongo dhaifu wa kilimo wamekuwa wakitoa elimu kwa wataalam wa kilimo na wakulima hasa vijana juu ya  kuboresha afya ya udongo kwa kutumia unga virutubishi  unaojulikana kitaalam kama limestone.
 
Alisema udongo ndio kila katika  kilimo kwa sababu ndio unaolea mazao tangu yanavyopandwa hadi kuvunwa hivyo ukiwa na afya njema mkulima ana uhakika wa kuwa na mazao yenye mengi na yenye ubora.
 


No comments:

Post a Comment

Pages